Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mei 18,2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, ametoa rai kwa wawekezaji na wafanyabiashara kuona umuhimu wa kufunga kamera za ulinzi ndani na nje ya viwanda, kuwa makini na makampuni ya ulinzi na kuajiri wafanyakazi waadilifu.
Aidha amewataka ,kutoa kipaumbele kwa masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo ya viwanda na biashara zao.
Morcase, alitoa rai hiyo wakati wa kikao kilichofanyika Mei 17 ,2025 kati yake na wamiliki wa viwanda pamoja na wafanyabiashara, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao za kiusalama na kuweka mikakati ya kuzitatua.
Alieleza, pamoja na jukumu la msingi la Jeshi la Polisi la kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, bado ni muhimu kwa wafanyabiashara kuchukua hatua za ziada katika kulinda maeneo yao.
Aliwaasa ,kujali wafanyakazi hao ili wajisikie kuwa sehemu ya taasisi na kushiriki kikamilifu katika kulinda mali.
Akitoa shukrani Mwakilishi wa Mmiliki wa Kiwanda cha Bagamoyo Sugar, Ramadhan Msika, aliiomba Polisi Mkoa wa Pwani kuendeleza utaratibu wa kutembelea viwanda kwa lengo la kutoa elimu ya ulinzi na usalama na kuimarisha doria katika maeneo hayo ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu.
Alimpongeza kamanda Morcase kwa kuandaa kikao hicho ambacho amedai kimetoa elimu muhimu na kutatua baadhi ya changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo.
Msika aliongeza kuwa ,anaamini mikakati iliyowekwa itatekelezwa kwa ufanisi na kuimarisha hali ya usalama katika maeneo yao ya kazi.
Kikao hicho ni sehemu ya mwendelezo wa mikutano inayoratibiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wazalishaji wa bidhaa za kilimo, maofisa usafirishaji, na wauzaji wa tiba asili, ili kuhakikisha elimu ya ulinzi na usalama inawafikia wananchi wa makundi yote.