Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA la Ujamaa Community Resource Team (UCRT) limefanikisha vijiji 18 vya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kupata hati ya matumizi ya ardhi baada ya kupimwa hivyo kuondokana na changamoto ya migogoro ya ardhi na uuzaji ardhi holela unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji wasiokuwa na uaminifu.
Pia, viongozi wa vijijini hivyo wamepatiwa mihuri ya moto na hati miliki za kimila kwa baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wakiwemo wanawake.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Raphael Lulandala akizungumza kwenye kijiji cha Lengasiti, amesema hatua hiyo iliyowezeshwa na shirika la Ujamaa Community Resource Team (UCRT), kwa ufadhili wa IUCN-ICI na PODONG itapunguza migogoro ya ardhi.
Lulandala amesema shirika la UCRT kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya hiyo na tume ya Taifa ya matumizi ya ardhi wamefanya kazi kubwa ya kihistoria.
“Jambo hili kubwa limeturahisishia na kutupunguzia migogoro ya ardhi kwani nitawachukulia hatua viongozi wanaouza ardhi kiholela bila kushirikisha mkutano mkuu wa kijiji,” amesema Lulandala.
Ametoa rai kwa mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka na Mwenyekiti wa CCM wilaya Kiria Laizer kutomwingilia pindi akichukua hatua kwa viongozi wanaojihusisha na uuzaji ardhi kiholela.
Amesema baadhi ya wanakijiji wanapewa maeneo na viongozi ila wanauza kisha wanarudi kuomba tena ardhi nyingine jambo ambalo siyo sahihi.
“Hata uuzaji wa ardhi vijijini mtu ananunua ekari 50 anaenda kwa mwingine anapata ekari 50 mwisho anakuwa na eneo kubwa kisha wanamlalamikia amehodhi ardhi,” amesema Lulandala.
Mratibu wa UCRT wa wilaya za Simanjiro na Kiteto, Edward Loure ametaja vijiji 18 vilivyonufaika na upokeaji vyeti, mihuri ya moto na hati miliki za kimila ni Lengasiti, Naisinyai, Naepo na Losoito.
Ametaja vijiji vingine ni Olchoro nyori, Magadini, Korongo, Ngorika, Lemkuna, Lormorjoi, Ngage, Naberera, Gunge, Loiborsoit B, Endonyo engijape, Orkirung’urung’ Irkujit na Nakweni.
Amesema changamoto iliyopo kwenye wilaya hiyo ni baadhi ya viongozi wa vijiji wasio waaminifu wanachangia kuzalisha migogoro ya ardhi.
“Unakuta kiongozi mwingine uchaguzi ukifanyika na kura zisipotosha anaondoka na vifaa na kuendelea kuuza ardhi kupitia mihutasari iliyopita ya vijiji,” amesema Loure.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema Mratibu wa UCRT Loure amekuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi.
Ole Sendeka amesema miongoni mwa wazalendo wa Simanjiro ambao atawazungumzia vyema popote ni pamoja na Loure kwani amechangia upimaji wa vijiji vingi.
Hata hivyo, amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafugaji na kutoruhusu maeneo yao ya malisho kugeuzwa kuwa mapori tengefu au mapori ya akiba.
“Tunamshukuru Rais Samia kwani amekonga mioyo ya wafugaji kwa kiruhusu hilo na pia nami nilisimama kidete kusema hilo japokuwa nilibezwa, nikang’ong’wa ila leo ardhi ya wafugaji imebaki salama kupitia yeye,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer amesema shirika hilo limefanya kazi ya kizalendo kwani migogoro ya ardhi iliyokuwa inasumbua imetatuliwa kupitia UCRT.
“UCRT imetekeleza kikamilifu ilani ya uchaguzi wa CCM kupitia matumizi ya ardhi na kusababisha kuepusha migogoro isiyo ya lazima,” amesema Kiria.
Mwenyeki wa kitongoji cha Edonyonapi Baraka Laizer amesema hatua hiyo ni nzuri kwa wakazi wa vijiji hivyo 18 kwani mpango huo wa matumizi bora ya ardhi itawaondolea migogoro.
Laizer amesema mpango huo ni mzuri kwani upo kwa kina na unaelezea matumizi ya maeneo ya makazi, malisho, kilimo na huduma za kijami.


