Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akiweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji Michiga ambao utahudumia zaidi ya wakazi 11,628 wa vijiji vitatu vya Michiga,Mnazimmoja na Pachani Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara,kulia Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Abdala Mwaipaya kushotoa,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa Kijiji cha Michiga Wilayani Nanyumbu Zuwena Kambutu mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji utakaogharimu kiasi cha Sh.milioni 310.
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Michiga Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara,wakichota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Wilaya ya Nanyumbu baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuweka jiwel la msingi ujenzi wa mradi wa maji Michiga utakaogharimu zaidi ya Sh.milioni 310.
Muonekano wa Tenki la kuhifadhi lita 50,000 za maji linalojengwa katika kijiji cha Michiga kwa ajili ya kuhudumian wakazi zaidi ya elfu 11 wa vijiji vya Michiga,Mnazimmoja na Pachani Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.
…….
Na Mwandishi Maalum, Nanyumbu
WANANCHI zaidi ya 11,628 wa vijiji vya Michiga,Mnazimmoja na Pachani Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara,wameanza kuwa na matumaini ya kuondokana na changamoto ya maji safi na salama baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini(Ruwasa) Wilayani humo kuanza ujenzi wa mradi wa maji ya bomba utakaogharimu Sh.310,034,722.20.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani humo Simon Mchucha, wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi.
Alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa Mwezi Mei 2024 na ulitarajia kukamilika mwezi Aprili 2025 lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza zikiwemo kuchelewa kwa malipo ya Mkandarasi na mvua,muda wa kutekeleza wake umeongezwa hadi Mwezi Julai mwaka huu.
Alisema,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 3,500 kwa saa ambacho kipo kijiji cha Mnazi mmoja.
Mchucha alisema,mradi huo ukikamilika utatoa huduma ya maji safi na salama katika vijiji hivyo na vijiji vya jirani na katika utekelezaji wa mradi wakazi 19 akti yao wanawake 5 na wanaume 14 wamefanikiwa kupata ajira za muda.
Kwa mujibu wake,mradi unatekelezwa kupitia program ya malipo kwa matokeo(PforR) kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 na Mkandarasi amelipwa Sh.152,434,916.92 kati ya fedha hizo Sh.39,411,193.50 malipo ya awali na Sh. 113,023,723.42 fedha za hati ya kwanza ya malipo.
Alisema,utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 81 na kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa nyumba ya uendeshaji wa pampu na uzio ambao umefikia asilimia 90,ujenzi wa tenki la lita 50,000,ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji,ununuzi na uletaji wa bomba mita 5,596 kuchimba mitaro na kulaza bomba pamoja na ununuzi na ufungaji wa pampu.
Mchucha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya awamu ya sita kuleta fedha hizo ambazo zinakwenda kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ali Ussi,amewapongeza wataalam wa Ruwasa kwa usimamizi mzuri na Mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa viwango vinavyotakiwa,hata hivyo amemuagiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi haraka ili wananchi wapate huduma ya maji.
Alisema,Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji ili kuwaondolea wananchi adha ya kukosa huduma za kijamii na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hizo.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Abdala Mwaipaya alisema,wananchi wa vijiji hivyo wana changamoto kubwa ya huduma ya maji safi na salama,hivyo mradi huo utakuwa suluhisho la changamoto ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu.