Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
BODI ya Ithibati ya Waandishi wa habari(JAB)imetoa rai kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo vya kihabari kuanza kujisajili rasmi kwenye mfumo kwani imeanza rasmi kutoa vitambulisho vya waandishi wa habari(Press Card) vitakavyowawezesha kufanya kazi zao kwa heshima na uadilifu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo May 16,2025 jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando amesema Kupitia ithibati, itaonesha waandishi wa habari wenye sifa stahiki na waliopata mafunzo yanayohitajika ili kufanya kazi kwa ufanisi na kusaidia kuimarisha weledi katika tasnia ya habari na kudhibiti usambazaji wa habari zisizo sahihi.
“Waandishi wa habari waliothibitishwa wanaweza kupata unafuu katika kupata habari kutoka kwa taasisi za serikali na sekta binafsi kwa kuwa wanatambulika rasmi.
“Kuwathibitisha (accredit) waandishi wa habari ni hatua muhimu katika kuhakikisha taaluma ya uandishi wa habari inazingatia viwango vya kitaaluma, maadili, na uwajibikaji,”alisema Mhando.
Amefafanua kuwa ithibati itasaidia kulinda haki na uhuru wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao.
Mhando ameongeza kuwa Waandishi wa habari wanaotambulika rasmi wana nafasi nzuri ya kulindwa dhidi ya vitisho, manyanyaso, na madhila wanayoweza kukumbana nayo kazini.
Kwa njia hiyo, ameongeza kuwa ithibati inakuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha mazingira salama ya uandishi wa habari.
“Kuthibitishwa au kupewa Ithibati na Bodi kunakuza hadhi na heshima ya taaluma ya uandishi wa habari. Kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama sheria na udaktari, uandishi wa habari unapaswa kutambuliwa rasmi kama taaluma yenye hadhi na umuhimu mkubwa katika jamii,”alisema.
Amesema ithibati itarahisisha kazi yao ya kukusanya na kusambaza habari sahihi kwa umma na kulinda usalama wao hasa wanapofanya kazi katika mazingira hatarishi kama vile migogoro au wakati wa uchaguzi.
Amesema maombi ya ithibati na vitambulisho (Press Cards) yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari unaolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.
“Waandishi wanapaswa kuingia kwenye kiunganishi https://www.taihabari.jab.go.tz na kufuata maelekezo ya kujisajili.
“Baada ya kujaza taarifa kwa usahihi, mwombaji atapokea msimbo (code) kupitia SMS na kiungo kwenye barua pepe ili kuendelea nahatua za kujaza wasifu, kufanya maombi, kupata ankara ya malipo, kulipia na kuwasilisha maombi ya kupata Kitambulisho (Press Card),”amesema.