WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,akiwasilisha leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026
Na.Alex Sonna-D0DOMA
WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 132.1 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi watalii 2,141,895 10 Mwaka 2024.
Hayo yameelezwa leo Mei 19,2025 bungeni Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo,Blaozi Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Waziri Chana amesema katika kipindi cha Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri na shupavu wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Muongoza Watalii Namba Moja nchini, Serikali imeendelea kutekeleza masuala mbalimbali katika sekta za uhifadhi na utalii.
“Na hakika tumeshuhudia mageuzi makubwa na mafanikio ya hali ya juu katika miaka hii minne na mwaka mmoja huu wa utekelezaji wa Bajeti,”amesema Waziri Chana.
Amesema idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 307.9 kutoka watalii 788,933 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 3,218,352 mwaka 2024.
“Hatua hii imewezesha idadi ya watalii kufikia 5,360,247 sawa na asilimia 107.2 ya lengo la watalii 5,000,000 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020.Kwa rekodi hizo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), limeitaja Tanzania kuwa nchi ilizoongoza Afrika kwa mwaka 2024.
“Kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya janga la UVIKO-19 ambapo utalii Tanzania ulikua kwa asimilia 48, Ethiopia (40%), Morocco (35%), Kenya (11%) na Tunisia (9%). Haya ni matokeo yaliyochagizwa na maono na kujitoa kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika filamu za Tanzani,”amesema Waziri Chana
mwisho