WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,akiwasilisha leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetaja vipaumbele 10 itakavyovitekeleza katika bajeti ya 2025/2026 ikiwemo kuendelea kujitangaza kupitia ligi mbalimbali duniani zenye kuangaliwa na watu wengi.
Vipaumbele hivyo vimetajwa leo bungeni Mei 19,2025 na Waziri wa Wizara hiyo Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo ni Pamoja na kuendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kupitia,matangazo katika ligi kuu za michezo mashuhuri duniani, mashindano ya kimataifa, mashirika ya ndege; misafara ya utalii; matamasha ya kimataifa na mitandao mbalimbali ya Kimataifa na Vyombo vya Habari.
Waziri Chana amevitaja vipaumbele vingine ni Kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo maeneo ya malikale pamoja na utalii wa fukwe na mikutano na matukio, meli, michezo, tiba na utamaduni.
Vipaumbe vingine ni Kuboresha miundombinu ya utalii na uhifadhi ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na huduma za utalii;Kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa uhifadhi na rasilimali, ufuatiliaji, utangazaji na uendeshaji wa shughuli za utalii na Kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale.
Waziri Chana ameeleza kuwa Wizara hiyo pia imejipanga kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya Misitu na Nyuki,Kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu mbalimbali, kufanya tafiti za kimkakati na kutoa huduma za ushauri zinazohusu masuala ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori, misitu na nyuki, malikale na uendelezaji utalii.