Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Ndg. Tido Mhando, ametoa onyo kali kwa watu wanaokusudia kutumia vyeti bandia katika mchakato wa kuomba kuthibitishwa kama waandishi wa habari kupitia mfumo mpya wa usajili wa kidijitali.
Akizungumza tarehe 19 Mei 2025 katika mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam, Mhando alisisitiza kuwa Bodi hiyo sasa itatoa vitambulisho vya uandishi wa habari (Press Cards) kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa TAI-Habari unaopatikana kupitia tovuti ya https://taihabari.go.tz.
“Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijitali. Maombi yatafanyika kupitia mfumo wa TAI-Habari,” alisema Mhando.
Alifafanua kuwa waombaji wanatakiwa kuwa na taarifa muhimu kama namba ya simu na barua pepe zinazofanya kazi, picha ya passport iliyoskaniwa, barua ya utambulisho kutoka taasisi wanakofanyia kazi au wanakowasilisha kazi zao (kwa waandishi wa kujitegemea), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), na ada ya shilingi 50,000.
Aidha, aliweka msisitizo kuhusu uwasilishaji wa vyeti halali vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na mamlaka husika—ikiwa ni TCU kwa vyuo vikuu na NACTVET kwa vyuo vya kati.
“Tafadhali sana, usiwasilishe cheti feki. Hii ni kinyume cha maadili ya taaluma ya habari na pia ni kosa la kisheria litakalodhibitiwa kwa mujibu wa sheria za nchi,” alionya.
Kwa mujibu wa Mhando, hatua hiyo inalenga kuboresha utoaji huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya uandishi wa habari, na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.
Aidha, aliwataka Wahariri, Waandishi na waajiri kushirikiana na Bodi kwa kutoa usaidizi katika kuimarisha maadili, weledi na uwajibikaji wa taaluma ya habari nchini.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, Wakili Patrick Kipangula, alijibu maswali ya waandishi kuhusu wale walioko kwenye tasnia bila kuwa na sifa za kitaaluma. Alisema kuwa Sheria iliwapa muda wa miaka mitano kujisomea na kutimiza vigezo, na baadaye Waziri kuongeza mwaka mmoja wa nyongeza. Hata hivyo, Kipangula alieleza kuwa hadi sasa miaka nane imepita na hakutakuwa na muda wa ziada tena.
“Kwa hiyo, ni muhimu kila mtu anayehusika kuhakikisha anatimiza vigezo vilivyowekwa ili kuendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na maadili ya taaluma,” alisisitiza.