WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,akiwasilisha leo Mei 19,2025 bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetaja mafanikio 10 iliyopata katika kipindi cha miaka minne ikiwemo kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii ambapo Serikali imeingiza Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.9 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa.
Mafanikio hayo yametajwa leo Mei 19,2025 bungeni Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo,Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Waziri Chana amesema Mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.9 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa.
Aidha, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Shilingi 11 bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 209.8 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 353.1.
“Hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nafasi ya tisa (9) duniani na kushika nafasi ya tatu (3) Barani Afrika kwa ongezeko la mapato ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya UVIKO-19,”amesema Waziri Chana.
Ameyataja mafanikio mengine ni Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali, Tanzania Imeendelea Kutambulika na Kung’ara Kimataifa, Kuimarika kwa Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori, Kuimarika kwa Biashara ya Mazao ya Misitu na Nyuki, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Kurejeshewa Hadhi ya Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai (UNESCO Global Geopark).
Mafanikio mengine ni Mafanikio ya 4R za Rais Samia Katika Kukuza Biashara ya Utalii kwa Kuiwezesha Sekta Binafsi, Kuandaa Tuzo za Kwanza za Uhifadhi na Utali, Mafanikio ya Mikakati Mahsusi ya Kutangaza Utalii.