.jpeg)
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ushauri ya Boston Consulting Group Ltd. Edward Lupasa akizungumza na Mwandishi kutoka Michuzi media (hayupo pichani)
JAMII imetakiwa kutambua kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri si ya Chama cha Mapinduzi (CCM), bali imetokana na mapato ya kodi zinazokusanywa na halmashauri hizo.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Boston Consulting group limited Edward Lupasa wakati akifanya mahojiano na Michuzi blogs kuhusu umuhimu wa mikopo hiyo kwa vijana na wanawake walioko kwenye vikundi vya ujasiriamali.
Amesema mikoa ya Iringa, Njombe,Singida na dar es salaam ni miongoni mwa maeneo yaliyokwisha kunufaika na mikopo hivyo, wananchi wanaopata mikopo hiyo wanapaswa kurejesha kwa wakati ili wengine nao waweze kunufaika.
“Ni vyema vijana wakaungana na kuunda vikundi vya ujasiriamali ili wanufaike na mikopo hii na kuondokana na wimbi la ukosefu wa ajira. Badala ya kusubiri kuajiriwa, wajiajiri ili waongeze kipato chao na kuchangia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Lupasa
Ameongeza kuwa Kampuni hiyo, kwa kushirikiana na Chuo cha Biashara (TIA), imepanga kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wanaohitimu vyuo ili kuwaandaa kujiajiri badala ya kufikiria tu kuajiriwa kwani nafasi za ajira ni chache huku waombaji wakiwa ni wengi.
“Kwa mfano, nafasi kumi za kazi zinapotangazwa, waombaji wanaweza kufikia zaidi ya laki mbili. Hii inaonesha ni kwa namna gani kuna haja ya kuandaa vijana kujiajiri wenyewe na kuondoa akili ya kujiajiri .Mpango huu wa mafunzo utasaidia sana kupunguza changamoto hiyo ya ajira,” ameeleza.
Amesema mafunzo hayo yatatolewa nchi nzima, ambapo yatakuwa bure kwa wanafunzi walioko vyuoni, lakini kwa wale waliopo nje ya mfumo wa elimu ya juu, watatozwa gharama nafuu ili kufanikisha huduma hiyo.
Aidha, Lupasa ameitaka jamii kuchukua mikopo katika kampuni au taasisi zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuepuka utapeli unaofanywa na baadhi ya watu wanaodai kutoa mikopo kwa masharti nafuu lakini kwa nia ya kuwalaghai wananchi.
“Lengo la kampuni yetu ni kuwasaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kusimamia biashara zao, kutafuta fursa za masoko na kuongeza ufanisi katika shughuli zao,” amesema.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kupunguza utegemezi, hasa miongoni mwa vijana, na hadi sasa wamefanikiwa kwa asilimia 100 katika kuwafikia vijana, ingawa bado wanakutana na changamoto katika kusaidia kwa kiwango cha juu kutokana na kuwashirikisha pia wazazi ambao mara nyingi ndiyo waliowekeza kwenye elimu ya vijana hao.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo imejikita katika kutoa elimu kuhusu ulipaji wa kodi kwa hiari, ili wafanyabiashara waweze kuepuka usumbufu kutoka kwa mamlaka husika, pamoja na kuhakikisha kuwa biashara zao zinakua na kuwa na sifa ya kukopesheka.
“Tangu kuanzishwa kwa kampuni hii, tumewasaidia zaidi ya wafanyabiashara 3,000 ambao wameweza kulipa kodi kwa hiari baada ya kupata elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa kumbukumbu. Wengi wao walikuwa hawana mpango mkakati wa biashara, lakini sasa wanauelewa vizuri na wanafanya biashara kwa ufanisi,” amesema.
Lupasa amesema kampuni hiyo hutumia mifumo mbalimbali ya kidigitali inayokidhi mahitaji ya biashara kulingana na sheria za bodi ya uhasibu, huku wakishirikiana na watoa huduma mbalimbali ili kuhakikisha mafanikio kwa wateja wao.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni usuasuaji wa baadhi ya wafanyabiashara katika kurejesha mikopo au kulipa ada za huduma, pamoja na dharau kutoka kwa baadhi ya wateja. Hata hivyo, kampuni hiyo inaendelea kupambana na changamoto hizo kwa lengo la kufungua fursa zaidi za uwekezaji ndani na nje ya nchi.