Kaimu Mkurugenzi Tiba, Wizara ya Afya, Dkt. Winifrida Kidima, akizindua rasmi mradi wa Enhancing Epilepsy Care in Africa (EECA) katika Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma. Uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa mpango wa kuboresha huduma za kifafa, kupunguza unyanyapaa na kuboresha maisha ya Watu Wenye Kifafa (WWK).
***
Dodoma, 20 Mei 2025 – Shirika la Amref Health Africa Tanzania (Amref Tanzania) kwa kushirikiana na Serikali kupitia wizara ya Afya limezindua rasmi mradi wa kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na kifafa pamoja na matatizo mengine ya mfumo wa fahamu. Mradi huo uitwao “Enhancing Epilepsy Care in Africa (EECA)” umezinduliwa katika mkoa wa Dodoma, ukilenga Wilaya za Bahi na Chamwino kama maeneo ya mfano kwa utoaji wa huduma jumuishi za kifafa zinazoendeshwa kwa kushirikisha jamii.
Mradi huu wa miaka mitatu, unaotekelezwa kuanzia Januari 1, 2025 hadi Desemba 30, 2027, Kwa ushirikiano kati ya Amref Tanzania, Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Asasi isiyokuwa ya Kiserikali inayojihusisha na kuijengea jamaa uelewa juu ya Kifafa Tanzania (TEA), Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya Wazazi wa Watoto Wenye Kifafa Tanzania (POCET), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu Antwerp cha Ubeligiji. Ufadhili wa mradi huu umetolewa na BAND Foundation na kuungwa mkono na UCB Innovation for Health Equity Fund.
Mradi unalenga makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo wananchi kwa ujumla, watu wenye kifafa, wazazi, walezi, familia, watoa huduma za afya, watunga sera, pamoja na viongozi wa kijamii.
Mpango huu ni mojawapo ya jitihada za Shirika la Amref Tanzania katika kushirkiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuboresha Mifumo Imara ya Afya (HSS) na Kuwawezesha Wananchi kwa lengo la kufanikisha huduma endelevu za afya zinazomlenga mwananchi.
Vilevile kuboresha huduma bora za kifafa na matibabu, kupitia mafunzo kwa wahudumu wa afya, kampeni za kupambana na unyanyapaa. Vilevile mradi unalenga kuboresha afya, ubora wa maisha na ujumuishwaji wa watu wenye kifafa pamoja na familia zao katika jamii husika.
“Mradi wa EECA ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dhamira ya Shirika la Amref Tanzania ya kushiriki katika kuimarisha mifumo ya afya na kuwawezesha wananchi,” alisema Dkt. Aisa Muya, Mkurugenzi wa Programu – Amref Tanzania.
“Kwa kuboresha huduma za kifafa katika mfumo wa afya ya msingi nchini, tutaboresha upatikanaji wa huduma za matibabu huku tukijenga uhimilivu na umiliki wa huduma hizi katika jamii. Hii ni sehemu ya mkakati wa Shirika katika kuboresha mifumo ya huduma za Afya kama kifafa. Mradi huu unaakisi mkakati wetu mpana wa Kuimarisha Mifumo ya Afya kwa kuwekeza katika rasilimali watu, matumizi ya takwimu, utoaji wa huduma, na uongozi wa kijamii ili kujenga mfumo wa afya jumuishi na wenye usawa zaidi.”
Akizindua rasmi mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Tiba, Wizara ya Afya, Dkt Winifrida Kidima, alieleza umuhimu mkubwa wa mradi huo kwa taifa.
“Mradi huu ni hatua ya mabadiliko katika namna tunavyokabiliana na matatizo mengine ya mfumo wa fahamu kama kifafa,” alisema Dkt. Kidima “Ni wajibu wetu kama jamii kushirikiana kuondoa unyanyapaa, kuvunja ukimya, na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma na msaada wa kijamii wanaohitaji.”
Mradi wa EECA utatekelezwa kwa kuzingatia mfumo wa huduma za afya ya msingi nchini (PHC), ili kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu, umiliki wa ndani na ulinganifu wa sera. Kipengele kikuu kitakuwa kuendesha kampeni dhidi ya unyanyapaa, kuhamasishaji jamii, pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa afya, wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs), walezi na viongozi wa kijamii.
MATOKEO YANAYOTARAJIWA:
👉Kipaumbele kikubwa kuboresha sera juu ya ugonjwa wa kifafa katika ngazi mbalimbali na taasisi.
👉Kuongezeka uelewa wa jamii juu ya ugonjwa wa kifafa na magonjwa ya neva na kupambana na unyanyapaa.
👉Kuimarishwa kwa kinga, utambuzi wa mapema na matibabu bora ya huduma za kifafa na magonjwa ya mifumo ya fahamu
Kuongeza upatikanaji wa dawa.
👉Matumizi bora ya takwimu za kisayansi na za kawaida katika kupanga sera na kuamua huduma bora za kifafa na neva.
KIFAFA: JANGA LISILOONEKANA LINALOHITAJI UAMUZI WA PAMOJA
Ingawa kifafa kinaathiri mamilioni ya watu duniani kote, mara nyingi huendelea kufichwa kutokana na unyanyapaa na kutoeleweka vizuri hasa katika maeneo yenye rasilimali finyu. Watu wanaoishi na kifafa nchini Tanzania hukumbana na changamoto nyingi si tu za kiafya, bali pia katika elimu, ajira, na maisha ya kijamii.
Kwa kuwekeza katika jamii na watu, mradi wa EECA unalenga kubadilisha simulizi hii kwa kuleta huduma bora za matibabu pamoja na kujenga mazingira ya heshima, ujumuishaji, na fursa mpya kwa watu wenye kifafa.
##################
KUHUSU AMREF HEALTH AFRICA TANZANIA
Amref health Africa Tanzania ni shirika la kitanzania lilioandikishwa kisheria tangu mwaka wa 1987 na lina bodi ya wakurugenzi inayojitegemea na linaongozwa na watanzania.
Kwa zaidi ya miaka 35, Amref Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi mbalimbali ya afya ya umma nchini Tanzania, ikishirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na wadau wengine muhimu katika Tanzania Bara na Zanzibar.
Amref Tanzania imekuwa ikiboresha huduma mbalimbali katika maeneo yaliyo pembezoni, kwa kuimarisha uhusiano kati ya jamii na mifumo rasmi ya afya, kuhimiza tabia za kuendeleza afya bora, kuzuia magonjwa, na kuwezesha wahudumu wa afya. Tunaongozwa na misingi ya uadilifu, ubora, utu (ubuntu), uwajibikaji na ushirikiano maadili yanayounda utamaduni wetu na kuelekeza hatua zetu.
Kwa sasa, Amref Tanzania inatekeleza miradi mbalimbali katika mikoa mingi ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mkakati wetu wa 2023–2030 unalenga kufanikisha huduma za afya kwa wote (UHC), kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya, kuelekeza nguvu kwenye usalama wa afya ya umma, kukabiliana na mabadiliko ya kidemografia, na kutumia fursa za data na teknolojia ya kisasa.
Programu zetu zinaweka kipaumbele kwa mbinu zinazozingatia jamii na mahitaji ya watu, kwa lengo la kufanikisha huduma endelevu za afya ya msingi na kushughulikia vichocheo vya kijamii vya afya.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na;
Eliminatha Paschal; Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Ushirikiano Amref Health Africa – Tanzania
Email: Eliminatha.Paschal@amref.org
Matukio katika Picha
Dkt. Aisa Muya, Mkurugenzi wa programu, Amref Tanzania, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa EECA. Mradi unalenga kuboresha utambuzi, matibabu na uondoaji wa unyanyapaa dhidi ya Watu Wenye Kifafa (WWK) katika wilaya za Bahi na Chamwino, kwa kuingiza huduma hizo ndani ya mfumo wa afya ya msingi nchini.
Viongozi kutoka Wizara ya Afya, wadau wa sekta ya afya, pamoja na washirika wa maendeleo katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa mradi wa Enhancing Epilepsy Care in Africa (EECA) jijini Dodoma. Mradi huo unalenga kuboresha huduma za kifafa na kuondoa unyanyapaa kwa Watu Wenye Kifafa (WWK) katika wilaya za Bahi na Chamwino, Dodoma