Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza moja ya vikao vya kikosi ambacho hatimaye kilitimiza azma yake mnamo Jumapili, Mei 18, 2025, kwa ushindi wa kishindo wa mgombea wa Tanzania Profesa Mohamed Yakub Janabi, alipopata kura 32 kati ya 47 zilizopigwa kwa siri na wajumbe wa nchi wanachama wa WHO Afrika, kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa WHO.
Dkt. Kikwete amepongezwa kwa kutumia umahiri na uhusiano wake wa kidiplomasia kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa, mchango ambao umetajwa kama kichocheo muhimu kilichowezesha Tanzania kupata ushindi dhidi ya wagombea kutoka Côte d’Ivoire, Guinea na Togo.
Uchaguzi huo umefanyika kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, mnamo Novemba 2024. Nafasi hiyo ilivuta wagombea mahiri kutoka mataifa kadhaa, lakini Profesa Janabi alifanikiwa kuungwa mkono kwa wingi, akionesha kuwa jina la Tanzania bado lina nguvu katika diplomasia ya afya barani Afrika.
Kwa mujibu wa taratibu za Shirika la Afya Duniani, jina la Profesa Janabi sasa litawasilishwa kwa ajili ya kuthibitishwa rasmi na Bodi ya Utendaji ya WHO katika kikao chake cha 157 kitakachofanyika Mei 28–29, 2025, mjini Geneva, Uswisi.