Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kusogeza huduma za kisheria kwa wananchi ambapo Ofisi inafanya Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida iliyoanza tarehe 19 na inaendelea hadi tarehe 25 Mei, 2025 katika viwanja vya Stendi ya zamani Manispaa ya Singida.
Akizungumza wakati wa Kliniki hiyo Mkurugenzi wa Divisheni ya Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria, Bi. Neema Ringo ameridhishwa na mwitikio wa wananchi wanaojitokeza kupata huduma mbalimbali katika kliniki hiyo, ambapo ameeleza kuwa masuala ya ajira, ardhi, ndoa na masuala ya kijinsia yamekuwa ni changamoto kwa wananchi wengi waliojitokeza katika kliniki hiyo.
*“Tukiwa katika siku ya tatu ya Kliniki yetu mwitikio ni mzuri wananchi wengi wamejitokeza kwa ajili ya kueleza changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili na eneo lililovuta watu wengi ni eneo la ardhi na Mawakili wetu wanaendelea kutoa huduma kwa kiwango kizuri.”* Amesema Bi. Ringo
Aidha, Bi. Ringo ametoa wito kwa wananchi waendelee kujitokeza zaidi katika Kliniki hiyo ili waweze kupata ya ushauri wa kisheria inayotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa wananchi wa Singida bila malipo.
*“Naomba nitoe wito kwa wananchi wa Singida waje kwa wingi kupata huduma yetu hii kwani tuna timu kubwa na nzuri ya Mawakili ambao wamejipanga vizuri kuwahudumia wananchi.”* Amesema Bi. Ringo
Kwa upande wake, mmoja ya wananchi waliopata huduma katika Kliniki hiyo, Bw. Julius Mkumbo amefurahishwa na huduma aliyoipata katika Kliniki hiyo ambapo amewapongeza Mawakili wa Serikali kwa kumuhudumiwa vizuri ndani ya muda mfupi.
*“Nimefika mahala hapa nikataja changamoto yangu nashukuru Mawakili niliowakuta hapa wamenihudumia vizuri sana na naona jambo langu sasa linaelekea kupata ufumbuzi nawashukuru sana.”* Amesema Bw. Mkumbo
Nae, Bi. Engeridi Makala ameushuruku uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta huduma hiyo ya kisheria mkoani Singida, kwakuwa huduma hiyo inatolewa bila malipo kwa wananchi hao huku akiamini suala hilo litawasaidia wananchi wengi wenye changamoto mbalimbali za kisheria.
*“Tunamshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutuletea huduma hii mkoani kwetu na kitu kizuri zaidi huduma hii inatugusa watu wa hali ya chini kwakuwa inatolewa bure kabisa”.* Amesema Bi. Makala
Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida ilizunduliwa rasmi tarehe 19 Mei, 2025 na inaendelea kufanyika hadi tarehe 25 Mei, 2025 ambapo wananchi wanapata huduma mbalimbali za kisheria katika viwanja vya Stendi ya zamani Manispaa ya Singida.