London
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Jiolojia ya Uingereza (BGS) zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya tafiti za madini.
Hati ya Makubaliano (MoU) hayo imesainiwa leo Mei 22, 2025 jijini London Uingereza na kushuhudiwa na Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo pamoja na Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Mbelwa Kairuki.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo ambayo pia yamefanyika Kwa njia ya mtandao, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Daniel Budeba amebainisha maeneo ya ushirikiano kuwa ni pamoja na kufanya tafiti za madini; vifaa vya teknolojia ya kisasa na uchunguzi wa sampuli za madini maabara.
Dkt. Budeba ametaja maeneo mengine ya ushirikiano ni kufanya miradi ya pamoja katika utafiti wa jiolojia, jiokemia, utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege, ugani wa jiolojia, ufuatiliaji na usimamizi wa masuala ya majanga asili ya jiolojia, usimamizi wa taarifa za jiosayansi na masuala ya kimazingira na mafunzo kwa watumishi na kubadilishana uzoefu.
Aidha, Dkt. Budeba ameongeza kuwa, makubaliano hayo yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili ambapo Tanzania itanufaika na ujuzi na teknolojia mpya katika kufanya tafiti za madini, huduma za maabara na usimamizi wa taarifa za jiosayansi.
Awali, akifungua hafla hiyo ya utiaji Saini Makubaliano hayo, Naibu Katibu Mkuu Mbibo amezishukuru pande zote mbili kwa kufanikisha kuandaa Hati hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha shughuli hiyo muhimu.
*#InvestInTanazaniaMiningSector*
*Vision2030:MadininiMaishanaUtajiri*