Na Mwandishi Wetu
BODI ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) Nchini, imetoa mwezi mmoja kuanzi kesho leo Mei 22 hadi Juni 21, 2025 kwa waandishi wote wa habari nchini kujisajili kupitia mfumo wa kidigitali wa TAI-Habari, ili kupata ithibati na vitambulisho rasmi vya kazi za kihabari, maarufu kama Press Card.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, .Patrick Kipangula, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa waandishi wote wa habari nchini wanatambulika kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.
“Waandishi wote wanapaswa kujisajili kupitia kiunganishi cha https://taihabari.jab.go.tz. Mwombaji anatakiwa kuwa na namba ya simu, barua pepe, na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA),” alisema Kipangula.
Aidha, waandishi wanatakiwa kuambatanisha viambatisho katika mfumo wa PDF vikiwemo picha ndogo (passport size), vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa, pamoja na barua ya utambulisho kutoka kwa taasisi wanayofanyia kazi au kwa waandishi wa kujitegemea (freelancers).
Taarifa hiyo imebainisha kuwa usajili huo unazingatia Kanuni ya 17(1)(a) ya Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, Tangazo la Serikali Na. 18 la Februari 3, 2017, inayowataka watendaji wa kazi za kihabari kupewa ithibati rasmi kabla ya kutekeleza majukumu yao.
Kwa kuzingatia kuwa mwaka huu kuna Uchaguzi Mkuu, JAB imeeleza kuwa ni lazima waandishi wote watakaoshiriki katika shughuli za uchaguzi wawe wamesajiliwa na kupatiwa ithibati ili kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kwa ulinzi wa kitaaluma.
Bodi pia imehimiza waandishi kutumia vizuri muda uliotolewa kukamilisha usajili huo. Ada ya ithibati ni shilingi elfu hamsini (50,000/=) inayolipwa kwa njia ya simu ili kurahisisha mchakato.
Usajili huo pia utaiwezesha Bodi kuratibu mchakato wa kuanzishwa kwa Baraza Huru la Habari kama inavyoelekezwa katika Kifungu cha 24 cha Sheria ya Huduma za Habari.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kusimamia uadilifu na weledi wa wanahabari, kuhakikisha wanatambulika rasmi, kuzingatia maadili ya taaluma, na kulindwa wanapotekeleza majukumu yao kwa maslahi ya jamii.