TAASISI ya Thabo Mbeki imeendesha mhadhara wake wa kila mwaka wa Siku ya Afrika hapa Tanzania, ikiwa ni hatua ya kihistoria ya kurejea katika nchi yenye uhusiano wa kihistoria na maisha ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.
Akizungumza katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Taasisi hiyo, Lukhanyo Neer, alieleza shukrani kwa mapokezi mazuri na kusisitiza umuhimu wa Tanzania katika safari ya maisha ya Mbeki kama mpigania uhuru.
“Mwaka 1962, Rais Mbeki alipoingia uhamishoni, aliondokea Dar es Salaam. Aliagwa uwanja wa ndege na Kenneth Kaunda pamoja na OR Tambo,” alisema Lukhanyo, akibainisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Mbeki na jiji la Dar es Salaam.
Taasisi ya Thabo Mbeki ilianzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuchochea ufufuo wa bara la Afrika kupitia mijadala, utafiti wa sera, na ushirikiano wa kijamii. Kila mwaka, Taasisi huadhimisha Siku ya Afrika kwa mfululizo wa mihadhara inayolenga kuendeleza mazungumzo juu ya maendeleo ya bara la Afrika na mwelekeo wake wa baadaye.
Baada ya kuandaa mhadhara wa 2023 huko Guinea-Conakry kwa mara ya kwanza nje ya Afrika Kusini, Taasisi hiyo imeichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa toleo la 2024/25 kuanzia tarehe 19 hadi 26 Mei.
Ratiba ya wiki nzima inahusisha mashauriano na vyuo vikuu, viongozi wa biashara, na wananchi wa Dar es Salaam na Morogoro. Jumanne, Taasisi ilishirikiana na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kujadili jinsi uchumi wa buluu na utalii vinavyoweza kuwa kichocheo cha mabadiliko ya bara.
Tukio la jana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lilijikita katika mijadiliano kati ya Rais Mbeki na wasomi pamoja na wanafunzi juu ya namna ya kuhuisha tena harakati za ufufuo wa Afrika.
Aidha Lukhanyo alikiri kuwa licha ya juhudi zilizofanyika kwa miaka mingi, Afrika bado haijafikia kiwango kinachotakiwa katika nyanja kama miundombinu, nishati, na maendeleo ya uchumi.
“Sote tunakubaliana kuwa bara hili halipo mahali tunapotamani. Swali kuu wiki hii ni: Nini kifanyike ili kuifufua tena Afrika?” Alihoji Lukhanyo
Shughuli za Taasisi zitaendelea leo Morogoro, mji wenye umuhimu wa kihistoria kwa Rais Mbeki wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi. Ijumaa, Taasisi itafanya mkutano na viongozi wa biashara wa Tanzania. Wiki hii itahitimishwa Jumamosi kwa mhadhara mkuu utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
“Kwetu sisi, mazungumzo ndiyo mwanzo wa kila suluhisho,” alisisitiza Lukhanyo. “Bila mazungumzo, hakuna suluhisho. Afrika Kusini isingepata ukombozi wake bila watu kukaa pamoja na kuzungumza. Ndiyo maana mihadhara hii ni muhimu ni fursa ya kutafakari kwa pamoja mustakabali wa Afrika tunayoitaka.”
Ziara ya Taasisi ya Thabo Mbeki ni ukumbusho wa dhima muhimu ya kihistoria ya Tanzania katika harakati za Uafrika na ni mwito kwa Waafrika wote kujitolea upya kwa ndoto ya bara lenye mafanikio, mshikamano, na kujitegemea.