WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei 23,2025 jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha miaka Minne ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,Zaidi ya viwanja 556,191 vimepimwa, mipaka ya vijiji 871 imehakikiwa, mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 846 imeandaliwa, na Hati za Hakimiliki za Kimila 318,868 zimesajiliwa.
Takwimu hizi zinaakisi jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kusimamia sekta ya ardhi na kuboresha maisha ya Watanzania.
Hayo yameelezwa leo Mei 23,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Deogratius Ndejembi,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana tangu mwaka 2021 hadi sasa, yakijikita katika uboreshaji wa sera, usimamizi wa milki, upangaji wa ardhi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
” Serikali imeandaa programu maalum ya uendelezaji upya wa maeneo chakavu katika miji mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za msingi, kuongeza fursa za kiuchumi, kupunguza umaskini na kuhakikisha miji inakuwa endelevu.”amesema Waziri Ndejembi
Aidha amesema kupitia programu hiyo, jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.349 katika mikoa 24 yameainishwa kwa ajili ya upangaji na uendelezaji. Kwa sasa, maeneo ya Makangira (Kinondoni), Maanga (Mbeya), Unga Limited (Arusha), na Igogo (Mwanza) ndiyo yameanza kutekelezewa mpango huo.
“Natoa wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa programu hii ili kuleta mapinduzi yatakayobadilisha mandhari na taswira za miji yetu,” amesema
Katika hatua nyingine, Serikali imekamilisha marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, na kuizindua rasmi tarehe 17 Machi 2025. Sera hiyo, iliyoboreshwa kuwa Toleo la Mwaka 2023, inalenga kuweka mfumo thabiti wa umiliki wa ardhi, kuhakikisha usawa katika upatikanaji, na kusimamia matumizi bora ya ardhi kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Waziri Ndejembi pia ametangaza kuanzishwa kwa Kitengo cha Milki, ambacho kinahusika na kusimamia sekta hiyo, kutoa elimu kwa umma na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau mbalimbali.
Aidha, amesema Serikali ipo katika mchakato wa kutunga sheria ya Milki itakayounda Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Milki (Real Estate Regulatory Authority) yenye jukumu la kuunda mfumo madhubuti wa usimamizi wa sekta hiyo.
Ili kufanikisha yote hayo,amesema Wizara imepokea shilingi bilioni 64.5 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika Halmashauri 131,Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 50 zimekopeshwa kwenye Halmashauri 57 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi (PDRF) ambapo Matokeo yake ni upangaji na upimaji wa viwanja 556,191.
Kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP), wizara imehakiki mipaka ya vijiji 871 na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 846 katika halmashauri 21ambapo Jumla ya vipande vya ardhi 583,734 vimepandishwa kwenye mfumo wa e-Ardhi huku hati 318,868 za kimila zimesajiliwa katika vijiji 236.
Amesema makazi 136,129 yamehalalishwa kupitia urasimishaji katika maeneo mbalimbali kama Jiji la Dodoma, Chalinze, Songea, Kahama, Kigoma, Shinyanga, Mtwara na Nzega.
Ndejembi amesema Wizara imefanya hatua kubwa kwenye matumizi ya teknolojia kwa kuweka alama 427 za msingi za upimaji katika halmashauri 35, kuanzisha vituo 22 vya kielektroniki vya upimaji ardhi, na kuandaa mfumo wa kidijitali wa vitalu vya thamani.
Halikadhalika, halmashauri 13 sasa zinatumia mfumo wa e-Ardhi, hivyo kuongeza ufanisi wa usimamizi wa taarifa za ardhi.
Licha ya hayo ameeleza kuwa Wizara imeendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa kama ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) na Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) kwa kupanga na kupima maeneo husika.
Waziri ametaja pia kukamilika kwa Mradi wa Morocco Square wenye thamani ya shilingi bilioni 137 ambapo nyumba zote 100 zimeuzwa, huku maeneo ya ofisi na biashara yakiwa yamepangishwa. Aidha, Mradi wa Kawe 711 wenye thamani ya shilingi bilioni 169 umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2025/2026.