* Asisitiza wazazi kutenga muda wa kuwa na watoto wao
* Asema familia imara ni msingi wa dunia imara
* Mashirika, Wadau wa Maendeleo waipongeza Serikali kuimarisha malezi ya watoto
* Zaidi ya kaya 15,000 zapata elimu ya malezi jumuishi na huduma za afya ngazi ya jamii
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa wazazi nchini kuvumiliana na kushirikiana katika malezi ya watoto wao ambao ndio msingi wa familia yeyote na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Mei 24, 2025 jijini Mwanza wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia yenye Kaulimbiu inayosema “ Mtoto ni Malezi: Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara”
“ Mtoto ni zao la matokeo ya wazazi wawili, Naomba wazazi tuthamini kuwa mtoto ni mtu muhimu na anahitaji kulelewa, jambo hili la kutolea watoto likiendelea tutakuwa na jamii isiyo na msingi imara wa familia,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kusema “ Na sisi tukumbuke kuwa tumefika hapa kwa kuwa wako wazazi walivumiliana na wakatulea katika familia, sisi tusiwe watu wa kutelekeza familia zetu, ni wajibu wa kila mmoja kujua kuwa familia ni msingi, tukijua kuwa kila mtu ana mapungufu hivyo tuvumiliane tulee familia zetu, ”
Dkt. Biteko amebainisha kuwa familia ikiimarika na dunia itaimarika hivyo wazazi watenge muda wa kuwa na familia zao ili kuwarithisha mila na tamaduni zao. Aidha, matokeo ya wazazi kushtakiana kwa watoto yanajenga chuki miongoni mwa watoto hata katika maisha yao ya baadaye.
Pia, ametoa rai kwa watoto kuwa watiifu kwa wazazi na walimu wao sambamba na kujifunza kwa bidii na kuishi kwa kufuata miongozo ya dini.
Katika kuadhimisha siku hiyo ya familia, Dkt. Biteko ametaja baadhi ya majukumu ya familia kuwa ni kutoa huduma ili kukidhi mahitaji ya watoto na familia, kusimamia malezi na makuzi mema ya watoto na kurithisha mila na tamaduni nzuri kwa watoto na familia kwa ujumla kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Fauka ya hayo, amesema katika kuimarisha malezi bora kwa watoto chini ya miaka 8, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeandaa na inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kipindi cha mwaka 2021/22 – 2025/26.
Programu ambayo inahakikisha kuwa watoto wanapata huduma stahiki na jumuishi za malezi kwa uwiano ulio sawa kuanzia mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake hadi anapofikisha umri wa miaka 8.
Ametaja mafanikio ya programu hiyo kuwa ni kuwajengea uwezo walimu wa awali 12,000 kutoka Halmashauri 184 kwa kutoa elimu ya malezi chanya ya watoto, wakihudumia zaidi ya watoto 360,000, kujenga vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 4,178, kutoa huduma za malezi na elimu ya awali kwa zaidi ya watoto 400,000. Aidha, vituo vya kijamii 206 vinavyomilikiwa na jamii yenyewe vimeanzishwa vikitoa huduma kwa watoto 11,675.
“ Katika kuimarisha huduma za kundi la watoto wa miaka 5 hadi 8, Serikali imejenga madarasa mapya ya awali 1,316 na kupatiwa vifaa vya kujifunzia. Pia, zaidi ya kaya 15,000 zimefikiwa na elimu ya malezi jumuishi na huduma za afya ngazi ya jamii wakipata huduma muhimu za afya, lishe, malezi yenye kuitikia hisia za mtoto, elimu ya awali na uchangamshi wa mtoto na ulinzi na usalama na mtoto, amesititiza Dkt. Biteko
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imetoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ya 15,000 wakiwemo Walezi wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana, Wahudumu wa Afya, Waandishi wa Habari, na Maafisa wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema kuwa Maadhimisho hayo yanalenga kutathmini nafasi ya familia katika malezi ya watoto ambao ndio msingi wa familia yeyote na Taifa kwa ujumla. Vilevile, malezi ya mtoto yanaanza mara tu mtoto anapozaliwa na Serikali inasisitiza baba na mama kuwa karibu na mtoto wakati huo.
“ Akina mama na akina baba washirikiane kwa pamoja kulea watoto ili wawe na malezi bora, wapate elimu na huduma zingine muhimu kwao,” amesema Mhe. Mwanaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amesema kupitia maadhimisho hayo wameandaa maazimio matano yanaloyenga kukuza malezi na makuzi ya mtoto ili kuimarisha familia.
Ametaja maazimio hayo kuwa ni kueneza vituo vya malezi na makuzi ya mtoto nchi nzima ili kila mtoto apate huduma jumuishi, lishe na kuwa na usalama wao pamoja na kufanya kazi kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Ameendelea kusema maazio hayo ni pamoja na kuimarisha huduma za utambuzi ili watoto wapate huduma mapema na kukuza eneo la smart malezi kwa kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili wazazi waweze kubadilishana mawazo kwa kutumia TEHAMA na watoto kupata nafasi ya kukua vizuri.
“ Kukuza na kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini na mila ili kuimarisha masuala ya malezi, makuzi na taasisi ya familia na kuongeza idadi ya watoa huduma wenye uwezo ili waweze kuenea nchi nzima,” amemalizia Dkt. Jingu.
Akitoa salamu za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Elizabeth Maganga amesema kuwa Mashirika hayo yameendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika malezi na makuzi ya mtoto nchini.
Amesema umri wa kisayansi wa kumlea mtoto ni mwaka 0 hadi 8 na kuwa ni kipindi kizuri cha kumsaidia mtoto kukua vizuri hivyo ni fursa kwa Taifa kuwekeza katika malezi ya mtoto.
Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Laximi Bhawan amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuweka mikakati ya kusaidia malezi ya watoto.
Aidha, pamoja na Maadhimisho hayo, Dkt. Biteko amezindua Miongozo ya Afua za Utekelezaji wa Malezi na Matunzo ya Watoto na Familia, Kutambua Mchango wa Wadau kwenye Malezi na Ustawi wa Familia na Kuzindua Kampeni ya Malezi kwa Mtoto