Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Prof. Tumaini Joseph Nagu kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni katika hafla iliyofanyika Ikulu.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Shaaban Kissu imesema Viongozi walioapishwa ni Prof. Tumaini Joseph Nagu aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya afya; Dkt. Blandina Buganzi Kilama aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu; na Jaji Mstaafu John Samweli Mgetta aliyeteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia aliwataka viongozi wateule kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu, huku wakishirikiana kikamilifu na watumishi watakaowakuta katika maeneo yao ya kazi.
Vilevile, Rais Dkt. Samia aliwasisitiza viongozi hao kuviishi viapo vyao kwa vitendo, wakizingatia nidhamu, maadili na uzalendo katika utumishi wa umma na kuwa mfano wa kuigwa katika uongozi bora na uwajibikaji kwa maendeleo ya Taifa.
Katika hatua nyingine, viongozi hao walikula kiapo cha maadili katika utumishi wa umma, wakiambatana na viongozi wengine wateule ambao ni Dkt. Fred Matola Msemwa, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango; Ndugu Lazaro Jacob Twange, aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO); na Ndugu Thadei Aldo Kabonge, aliyeteuliwa kuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Blandina Bugazi Kilama kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.
Viongozi wateule wakiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Jaji Mstaafu John Samweli Mgetta kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.