Wataalamu kutoka Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) kwa kushirikiana na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) wakifanya majaribio ya njia mpya ya kusafirisha umeme kutoka Ipole, Sikonge hadi Inyonga, kabla ya kuwasha rasmi kwa matumizi ya wananchi, tukio hili limefanyika Mei 24, 2025 katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Inyonga, Mkoani Katavi.
Wafanyakazi wa Kampuni ya ETDCO na TANESCO wakiwa katika picha ya pamoja katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Inyonga, Mkoani Katavi.
………………
Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa laini mpya ya umeme ya kilovolti 132 kutoka Ipole, Wilaya ya Sikonge, Tabora hadi Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.
Laini hiyo yenye urefu wa kilomita 133 iliyowashwa, ni hatua muhimu ya kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza.
Akizungumza wakati wa kuwasha laini hiyo katika kituo cha kupoza umeme cha Inyonga Mkoani Katavi, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, CPA Sadock Mugendi, amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, huku akiishukuru serikali na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kuiamini kampuni hiyo kutekeleza mradi huo wa kimkakati.
Mhandisi wa Mradi kutoka TANESCO, Mhandisi Dalali Lunyamila, amesema kituo cha Inyonga kina uwezo wa kupokea Megawatts 12, ambapo mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Mlele ni Megawatts 4, na hivyo kufanya uwepo na ziada ya Megawatts 8 ya matumizi ya sasa na baadaye.
Mhandisi Lunyamila amesema kuwa wananchi wa Wilaya ya Mlele na Majimoto wanatarajiwa kupata huduma ya umeme wa uhakika kupitia gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza na kusaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Dismas Massawe, amesema kuwa laini hiyo itakuwa kwenye kipindi cha matazamio kwa saa 48 kabla ya kuanza kutumika rasmi.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupeleka umeme wa uhakika wa grid kwenye maneneo ambayo yalikuwa hayajaonganishwa na grid kama vile Katavi kwa lengo la kuchochea maendeleo kwa kutumia Nishati safi, salama, na rafiki kwa mazingira.