Na Mwandishi Wetu, OR- TAMISEMI
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasilino Serikali na Msemaji Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI, John Mapepele ametoa wito kwa Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kutanguliza uzalendo na weledi wakati wa utoaji wa taarifa ili habari hizo ziwe na tija kwa taifa.
Mapepele ametoa wito huo mwisho wa juma wakati akiwasilisha maada kuhusu Mawasilino ya Kimkakati ya Kutangaza Nafanikio ya Sekta za Afya, Elimu na Miundombinu chini ya TAMISEMI kwa Maafisa Habari zaidi ya 200 wa Mikoa na Halmashauri zote nchini jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha siku mbili kwa MaafisaHabari hao kilichoratibiwa na Wizara hiyo.
Kikao kazi hicho kilichofunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe.Mohamed Omary Mchengerwa na kufungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa kimejadili pamoja na mambo mengine, mikakati mbalimbali ya kutangaza mafanikio ya Serikali, pia kuwajengea uwezo Maafisa Habari hao kwa mada mbalimbali za kitaaluma hususan matumuzi ya mifumo ya kidigitali kwenye utoaji wa taarifa na kuja na maazimio kadhaa ya kuboresha utendaji kazi.
Aidha, Mapepele amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika mikoa na Halmashauri zote nchini ambayo haijatangazwa ipasavyo na Maafisa Habari katika maeneo hayo na kuwataka kuwa wabunifu wa kutoa taarifa hizo
“Ndugu zangu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu ambapo tumeshuhudia mabarabara, madaraja, vituo vya mabasi na masoko yakitengenezwa kila uchao, ukiachia mbali madarasa, zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba kwenye kila kona hivyo ni wajibu wetu sisi Maafisa Habari wa Halmashauri na Mikoa kuwa wazalendo na kuisemea Serikali yetu ili wananchi waweze kujua na kutumia huduma hizi kikamilifu”. Amefafanua Mapepele
Akifungua kikao kazi hicho Mhe. Mchengerwa amewataka Maafisa Habari wote wa TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi kwa wakati za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ya kazi.
“Mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi hivyo msiache watanzania walishwe habari potofu”. Amesisitiza Mhe. waziri Mchengerwa
Akifunga kikao kazi hicho, Katibu Mkuu Msigwa ameipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kuratibu kikao kazi hiki ambapo ameshauri kiwe kinafanyika kila mwaka ili kufanya tathmini wa utendaji wa kazi na kujadiliana masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi wa kundi hili kubwa la Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri nchini katika kutoa taarifa za miradi ya maendeleo.