MBEYA-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewakaribisha wananchi wa Mbeya na viunga vyake katika banda lao lililopo Maonesho ya Mbeya City Expo ili waweze kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika ikiwemo nyumba za kisasa.
Wito huo umetolewa leo Mei 26,2025 na Afisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Daniel Kure katika viwanja vya Uhindini jijini Mbeya.
Maonesho hayo ambayo yalianza Mei 23,2025 huku yakitaraiwa kufikia tamati Mei 31,2025 yamefunguliwa rasmi leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Dkt.Juma Zuberi Homera.
Kure amesema, katika maonesho hayo ambayo yanazikutanisha taasisi mbalimbali za umma na zisizo za umma wananchi wakifika banda la NHC watapata taarifa sahihi kuhusu huduma wanazotoa na namna wanavyoweza kushiriki katika manunuzi ya nyumba.
Pia, watapata fursa ya kuijua miradi ya shirika ikiwemo NHC 711,Samia Housing Scheme Phase II kwa Dodoma na Dar es Salaam, Dodoma kuhusu mradi wa Medeli na Dar es Salaam ni Kijichi na Kawe.