*Mkuu wa Mkoa akagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa na NSSF na utakaoendeshwa na RADISSON na kujionea chumba cha mfano
Na MWANDISHI WETU,
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mradi wa hoteli ya nyota tano inayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuendelea kutekelezwa katika eneo la Capripoint jijini Mwanza. Hotel hiyo itakapokamilika itaendeshwa na kampuni ya kimataifa ya RADISSON.
Mhe. Mtanda alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, ambapo aliipongeza NSSF kwa uwekezaji huo mkubwa ambao utakapokamilika utakuwa na tija kwa Taifa kwa kuchochea shughuli za utalii na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
“Tayari chumba cha mfano ambacho ni hitaji muhimu kimekamilika, kikionesha mwonekano wa kuvutia unaotarajiwa kwa vyumba vyote, ambavyo vitakuwa na mandhari ya kuvutia ya Ziwa Victoria”, alisema Mhe. Mtanda.
Akiipongeza NSSF kwa uwekezaji huo kuwa ukikamilika utaongeza mapato ya Serikali, utachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kupitia huduma za utalii, ajira na malazi.
Kwa mujibu wa Mhe. Mtanda, Mkoa wa Mwanza kwa sasa unachangia asilimia 7.2 ya pato la Taifa, lakini anatarajia mchango huo kupanda hadi kufikia asilimia 10 baada ya kukamilika kwa miradi ya kimkakati ukiwemo wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwanza, meli ya Mv. Mwanza na reli ya SGR.
Akielezea umuhimu wa uwekezaji huo, Mhe. Mtanda alisema uwepo wa hoteli ya kiwango cha kimataifa ni hitaji la msingi kwa miji inayokua haraka kama Mwanza, hivyo utakapokamilika utachochea fursa za kiuchumi na kukuza utalii.
Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa NSSF, Bw. Gabriel Silayo, alisema Radisson tayari inaendesha hoteli zaidi ya 12,000 duniani, zikiwemo zaidi ya 98 barani Afrika, jambo linalowapa uhakika wa mafanikio ya mradi huo.
“Tumefanya utafiti wa kina na tunajua mradi huu utaleta faida kubwa si tu kwa NSSF kama mwekezaji, bali pia kwa wananchi kupitia ajira, kodi, na kukuza uchumi wa ndani,” alisema Bw. Silayo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo kutoka Afrika Kusini, Bw. Gehan Nel alisema atahakikisha anasimamia mradi vizuri ili kukidhi ubora wa hoteli zingine za RADISSON duniani na amepongeza serikali ya Tanzani kwa kuruhusu wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Alisema kwa kushirikiana na NSSF atasimamia mradi huo ili ukamilike kwa haraka kwani hoteli hiyo imejengwa katika mandhari ya kuvutia kando ya Ziwa Victoria na itachochea wageni wengi kufika nchini.
Uwekezaji huu ni moja kati ya majukumu ya Mfuko wa NSSF kuwekeza
sehemu mbalimbali ili kuhakikisha inalinda thamani ya michango ya wanachama.