Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA Akipata ufafanuzi kutoka kwa Meneja wa TFRA Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya wa kahawa iliyokobolewa kutoka katika _CPU central pulpery unit_ na baadae kuanikwa katika kichanja tayari kwa kupelekwa katika viwanda vya kukoboa kahawa na baadaye kuuzwa mnadani. Wajumbe wa bodi ya TFRA Dkt. Peter Shimo ( kushoto) na Hadija Jabir wakifurahia matunda yaliyosheheni kwenye mti wa kahawa wakati wa ziara ya kikazi kwa mkulima LOHE TANZANIA LIMITED, tarehe 27 Mei, 2025 Mbinga mkoani Ruvuma
Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo akiwa katika picha na wajumbe alioambatana nao wakati wa ziara yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku katika mazao ya kimkakati ya kahawa na parachichi kwa mikoa ya nyanda za juu kusini, ikiwa ni mkoa wa Ruvuma tarehe 27 Mei, 2025
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo akizungumza na wajumbe wa Bodi wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Mbinga (MBIFACU) Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma tarehe 27 Mei, 2025.
Wajumbe wa bodi ya TFRA, Dkt. Peter Shimo (kulia) akifuatiwa na Lilian Gabriel na Hadija Jabir (Kushoto) wakimsikiliza Meneja wa shamba la kahawa lenye ukubwa wa ekari 113 linalomilikiwa na kampuni ya LOHE Tanzania Limited, Regnald Mapunda wakati wa ziara ya bodi tarehe 27 Mei, 2025
Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo wa pili kutoka kushoto akiwa na wajumbe wa bodi, menejimenti ya TFRA na Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Miwa mara baada ya kikao kilichofanyika katika ukumbi wao wa mikutano Mbinga mkoani Ruvuma tarehe 27 Mei, 2025
……………….
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amewataka wakulima wa Kahawa Mbinga Mkoani Ruvuma kuzingatia kanuni na teknolojia bora za kilimo cha kahawa ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji, fursa ya kujiajiri na kuondokana na umaskini.
Dkt. Diallo ametoa ushauri huo tarehe 27 Mei, 2025, Mkoani Ruvuma ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Bodi ya TFRA kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa (MBIFACU), lengo kuu likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku katika mazao ya kimkakati ya kahawa na parachichi kwa mikoa ya nyanda za juu kusini.
Dkt. Diallo amesema, gharama na nguvu anayoitumia mkulima kuwekeza kwenye ekari moja ya shamba la kahawa, lazima ilingane na thamani ya uzalishaji anaoutarajia ambao ili kuupata ni lazima mkulima azingatie kutumia maarifa na sayansi katika uzalishaji wa zao hilo.
Aidha, Dkt. Diallo amewasihi wakulima kuondokana na tabia ya kukalili majina ya mbolea na badala yake wazingatie aina ya virutubisho vinavyohitajika kwenye mashamba yao na kununua mbolea yenye sifa zinazoendana na mahitaji ya udongo wa shamba lake.
Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya mbinga, Kanisius Marco, Dkt. Diallo alimuomba kufuatilia taarifa ya wakulima waliopimiwa afya ya udongo na maafisa kilimo waliowezeshwa kwa vifaa hivyo (Soil Scanner) ili kuwasaidia wakulima kuondokana na hasara ya kutumia mbolea kimazoea na kuishia kupata hasara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kanisius Marco ameeleza kuridhishwa na ushirikiano baina ya TFRA na watendaji ngazi ya Mkoa, Wilaya hadi vijiji unaowezesha kuwafikia wakulima na kutatua changamoto zao huku akikiri tangu afike wilayani hapo hajakutana na changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo wa Mkoa wa Ruvuma, Afisa Kilimo Onesmo Mpuya, ameishukuru Serikali kwa mpango wa ruzuku, akisema kabla ya mpango huo walikuwa wakikadiria kiwango cha matumizi ya mbolea kwa wakulima wao, lakini sasa kupitia mfumo wa pembejeo za kilimo, wanaweza kupata taarifa sahihi za matumizi na kufanya makadirio sahihi kwa misimu inayofuata ya kilimo.
Naye Michael Kanduyu Mwenyekiti wa MBIFACU ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza mpango wa mbolea ya ruzuku iliyowezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 16,000 hadi kufikia tani 24,000.