Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomiu
akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28,2025, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yatafanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WANANCHI wamekaribishwa kuhudhuria maonesho ya wiki ya Utumishi wa Umma katika viwanja vya Chinangali Park kuanzia Juni 16-23 Juni, 2025 ambapo huduma mbalimbali zitatolewa.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 28,2025 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma,Juma Mkomi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya siku ya Utumishi mwaka 2025.
Katibu Mkuu amesema Katika maadhimisho ya mwaka huu, Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Taasisi za Umma zitafanya maonesho na kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma kuanzia tarehe 16-23 Juni, 2025.
Aidha, katika maonesho hayo, huduma mbalimbali zitatolewa papo kwa hapo ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa (NIDA), hati za viwanja, kupima afya kutoka Hospitali za Benjamin Mkapa, Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JKCI), Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI). Vile vile kutakuwepo na huduma ya Gazeti la Serikali
Amesema maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo:”Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”
“Binafsi niwahakikishie kuwa, Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kushirikiana nanyi ili umma wa watanzania upate habari sahihi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ofisi yangu ili wananchi wanufaike na huduma zinazotolewa katika taasisi,”amesema Bw.Mkomi
Akiizungumzia siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni siku maalum ya Watumishi wa Umma ambayo husherehekewa Tarehe 23 Juni kila mwaka na Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya Nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.
Amesema Chimbuko la Sherehe hizi ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers Nchini Morocco mwaka 1994.
Amesema uamuzi huo ulizitaka Nchi za Afrika kusherehekea siku hii kwa kauli mbiu moja katika Bara zima la Afrika.
Aidha, Mkutano wa nne wa Mawaziri wenye dhamana na Utumishi wa Umma uliofanyika Mwezi Mei 2003 uliamua kuwa Siku ya Utumishi wa Umma iwe ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Utawala Bora na Utumishi wa Umma chini ya Umoja wa Afrika (AU).
Katibu Mkuu amesema katika kufikia Siku ya Utumishi wa Umma, shughuli mbalimbali hufanyika ikiwemo Watumishi wa Umma kufanya maonesho.
Pia, Kutambua mchango na umuhimu wa Watumishi wa Umma katika kuleta maendeleo kwenye Nyanja mbalimbali za maendeleo katika Mataifa yao.
Aidha,Kuwezesha Watumishi wa Umma kutambua Dira, Dhima, Malengo; Programu, Mikakati; Mafanikio na Changamoto zinazokabili Utumishi wa Umma
“Kuhamasisha na kuwapa motisha Watumishi wa Umma waendelee na kazi yao nzuri ya ujenzi wa Taifa na kuendelea kuwa wabunifu ili kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Vilevile,kupata mrejesho kutoka kwa wateja/wananchi na wadau wanaowahudumia
“Kuandaa Utumishi wa Umma ili uweze kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo siku za usoni,”amesema
Amezitaja faida nyingi zinazotokana na Siku ya Utumishi wa Umma, miongoni mwa faida hizo ni wananchi kupata fursa ya kufahamu wajibu wao na haki zao ili pindi wanapokosa haki zao waweze kujua namna ya kuzipata.
Pia Taasisi za Umma kupata fursa ya kubadilishana uzoefu juu ya mbinu na mikakati mipya ya namna ya kutoa huduma bora kwa Umma;
Vilevile,Taasisi za Umma kupata fursa ya kuonyesha ubunifu waliofanya katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma na kuondoa urasimu usiokuwa wa lazima katika michakato mbalimbali ya utoaji huduma.
Pia,Taasisi za Umma kupata fursa ya kupokea ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Wananchi, AZAKI, na Sekta Binafsi juu ya namna bora ya kuboresha utoaji huduma.
Vilevile,Taasisi kupata mrejesho na kuutumia mrejesho huo kurekebisha kasoro za utendaji zinazosababisha malalamiko ya wateja ili huduma za Serikali ziboreshwe kukidhi matarajio ya Wananchi.