Mwananchi mzalendo nchini Tanzania ameiomba Serikali Kuu kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo uchimbaji holela wa mchanga katika maeneo yasiyo rasmi Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani, hali ambayo imesababisha taharuki kwa wakazi wa maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mzalendo Francis Maigua amesema kuwa katika Wilaya ya Mkuranga kuna eneo lenye zaidi ya ekari 100 ambapo watu wamekuwa wakichimba mchanga kiholela kwenye maeneo ya makazi ya wananchi, huku Jeshi la Polisi likidaiwa kushindwa kuchukua hatua stahiki dhidi yao.
Maigua ameeleza kuwa licha ya juhudi zilizofanyika za kuwakamata wahusika na kuwapeleka Polisi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria, bado wamekuwa wakiachiwa huru bila kufikishwa Mahakamani.
“Mimi ni mzalendo niliyekubali kuteseka kwa ajili ya kuwatetea wananchi wezangi. Wakati mwingine nimekuwa nikikamatwa na kuteswa bila sababu ya msingi,” amesema Maigua.
Aidha, amedai kuwa tayari amepeleka taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, lakini mpaka sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahalifu hao.
Maigua amefafanua kuwa baadhi ya wahusika wa uhalifu huo wamekuwa wakitoa rushwa kwa viongozi wenye mamlaka ili kuepuka kuchukuliwa hatua.
Ameeleza kuwa tayari amewasilisha taarifa hizo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili hatua stahiki zichukuliwe.