Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
INGAWA kazi ni nguzo muhimu ya ustawi wa maisha ya binadamu, haitakuwa na maana endapo itaambatana na madhara ya kiafya au vifo. Usalama mahali pa kazi ni jambo lisiloepukika katika kujenga jamii yenye afya bora na taifa lenye uchumi imara.
Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2025 katika Kongamano la Afya na Usalama Kazini lililofanyika leo jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya afya na ajira kwa lengo la kujadili namna bora ya kulinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi kazini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Jerome Materu, alisema kuwa elimu ya kudhibiti vihatarishi kazini ni muhimu kwa ustawi wa mfanyakazi na taifa kwa ujumla.
“OSHA imepewa jukumu la kutathmini na kudhibiti vihatarishi vinavyotokana na kazi. Tunahimiza wadau na sekta zote, hasa zile zisizo rasmi, kujisajili ili kulindwa kisheria na kiafya,” alisema Materu.
Aliongeza kuwa ajali kazini husababisha madhara kwa mfanyakazi, upotevu wa kipato, gharama kwa waajiri, pamoja na adhabu au faini kutoka kwa mamlaka. “Lengo letu ni kuhakikisha mfanyakazi anakuwa na afya njema ili awe na tija kwa kampuni na taifa kwa ujumla,” alisema.
Materu alibainisha kuwa OSHA inatoa elimu na vifaa kinga bila malipo kwa sekta zisizo rasmi, huku akitoa rai kwa wadau kujitokeza na kujisajili ili kulinda afya zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Joseph Kilago, alisema serikali inawekeza katika usalama kazini ili kupunguza mzigo wa huduma za afya unaotokana na magonjwa yatokanayo na kazi.
“Msingi mzuri wa afya kazini huanzia ngazi ya chini. Kila mtu anapaswa kuhakikisha mazingira yake ya kazi ni salama. Magonjwa haya huanza taratibu na si rahisi kuponyeka,” alisema Kilago.
Alitolea mfano tofauti za vihatarishi kazini, akisema wachimbaji migodini hukumbwa na hatari tofauti na wale wa sekta zingine. “Serikali inaweka miongozo ya kisekta, na tumeshuhudia utekelezaji wake ukiimarika,” aliongeza.
Profesa Simon Mamuya wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya cha Muhimbili (MUHAS), alisema kuwa utafiti unaonesha uelewa mdogo wa madhara ya vitendea kazi miongoni mwa Watanzania, hasa katika sekta ya kilimo na uchimbaji.
“Wakulima wengi hawajui madhara ya viuatilifu wanavyotumia, vivyo hivyo wachimbaji wadogo hawajui athari za kuvuta hewa yenye sumu migodini. Matokeo yake, wengi hufariki wakiwa na umri mdogo,” alisema Profesa Mamuya.
Alisisitiza haja ya ushirikiano kati ya watafiti na watunga sera katika kutoa elimu na kuhakikisha matumizi salama ya zana za kazi.
Naye Dk. Israel Nyarubeli, Mkuu wa Idara ya Afya na Usalama Kazini wa MUHAS, alisema kongamano hilo lina umuhimu mkubwa kwa kuwa limewakutanisha wataalamu, watafiti, walimu na wadau wengine katika sekta hiyo.
“Maadhimisho haya yanatukumbusha historia ya taaluma hii nchini. Tangu miaka ya 1990 hadi kupitishwa kwa sheria ya afya na usalama kazini mwaka 2003, tumepiga hatua kubwa,” alisema Dk. Nyarubeli.
Alibainisha kuwa kongamano hilo pia lilitambua mchango wa waasisi wa taaluma hiyo kwa kuwapatia tuzo, akimtaja Profesa Mamuya kama mmoja wa waliotunukiwa heshima hiyo.
Aidha, alisema sehemu ya pili ya maadhimisho imejumuisha mijadala ya kisera, mawasilisho ya kisayansi, na tafiti kuhusu kinga dhidi ya ajali kazini. Alihitimisha kwa kutoa wito kwa waajiri kuwajali wafanyakazi wao kwa kuwaelimisha na kuwakinga dhidi ya vihatarishi kazini.
“Ni wakati wa kazi kuwa baraka kwa mfanyakazi, sio laana,” alisisitiza Dk. Nyarubeli.
