Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bw. Christian Nyakizee akizungumza na waandishi wa habari leo, Mei 29, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025
……………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi 202,571,047,774.96, kati ya miradi hiyo, miwili yenye thamani ya shilingi 194,489,926,994.09 imebainika kuwa na mapungufu, ikiwemo kuchelewa kukamilika kwa sababu ya ucheleweshwaji wa fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mei 29, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Bw. Christian Nyakizee, amesema kuwa miradi hiyo imehusu sekta za miundombinu (barabara), elimu na maendeleo ya jamii.
Bw. Nyakizee ameeleza kuwa katika kipindi hicho, TAKUKURU kwa kushirikiana na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imeshiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria ya mwaka 2025 yaliyoongozwa na kaulimbiu: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
“Pia, tumefanya uchambuzi wa mifumo mbalimbali ili kubaini mianya ya rushwa katika maeneo ya kiutendaji ndani ya ofisi, taasisi, idara mbalimbali, na kuchukua hatua za kuzuia hasa katika makadirio na makusanyo ya mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni,” amesema Bw. Nyakizee.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikia wananchi katika kata saba kupitia vikao na wadau mbalimbali, ambapo jumla ya kero 49 zimeibuliwa na kati ya hizo, 31 tayari zimepatiwa ufumbuzi.
Katika juhudi za kutoa elimu kwa umma, TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni imefanya semina 23, mikutano ya hadhara 24, vipindi mbalimbali vya redio na televisheni, kuimarisha klabu za wapinga rushwa 32, kuandika makala, pamoja na kushiriki katika maonesho saba.
Bw. Nyakizee pia amebainisha kuwa taasisi hiyo ilipokea jumla ya malalamiko 120; kati ya hayo, 76 yalihusiana na rushwa na 44 hayakuhusu rushwa.
Aidha, mashauri mapya sita yamefunguliwa katika Mahakama ya Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo, kati ya mashauri hayo, Jamhuri imeshinda shauri moja na kushindwa mashauri mawili.
Bw. Nyakizee ameeleza kuwa mikakati ya taasisi hiyo kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, na kuwahamasisha kushirikiana na TAKUKURU katika kutokomeza vitendo vya rushwa kuanzia sasa, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.