Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Bw. Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji wa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2025.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, imewafikisha mahakamani watuhumiwa 12 kwa makosa ya uhujumu uchumi, ubadhirifu na utakatishaji wa fedha kiasi cha shilingi 165,102,450.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa kutoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Bw. Holle Makungu amesema kuwa watuhumiwa hao wamefunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.
Bw. Makungu amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Annie Nyabugumba Maugo (Afisa Hesabu, OR-TAMISEMI), Tumsifu Christopher Kachira (Afisa Hesabu Mwandamizi, OR-TAMISEMI) pamoja na Aidanı Zabron Mponzi (Afisa Hesabu, OR-TAMISEMI).
Watuhumiwa wengine ni Jonathan Stanley Manguli (Afisa Hesabu), Godfrey James Martiny (Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu), Juvenalis Mauna (Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira), Josephat Mtembei (Mhandisi), Bibiana Moete (Mtunza Bohari), Henry Herman (Afisa Ugavi)
“Pia Wakandarasi watatu wameunganishwa katika kesi hiyo ambao ni Hamis Kashinje Manfred, Paulo Sam Mwakyusa, Godwin Adamson Cheyo ambapo Makampuni yao yanatuhumiwa kutumika katika utakatishaji wa fedha hizo” amesema Bw. Makungu.
Bw. Makungu ameeleza kuwa mashtaka dhidi ya watuhumiwa yamesomwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Bi. Neema Kazoka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Nestory Baro.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa wanakabiliwa na kosa la kusababisha hasara, kinyume na kifungu cha 10(1) cha Jedwali la Kwanza pamoja na vifungu vya 57 na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya 2022).
Kosa la utakatishaji fedha, kinyume na vifungu vya 12(1)(a) na 13(1)(a) vya Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sura ya 423 (Marejeo ya 2022) pamoja na kosa la ubadhirifu, kinyume na kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329
“Watuhumiwa wote wamepelekwa mahabusu kwa kuwa makosa yao hayana dhamana, Kesi yao itatajwa tena tarehe 12 Juni, 2025,” amesema Bw. Makungu.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Temeke imetekeleza ufuatiliaji wa miradi 13 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 11,229,346,597, Kati ya hiyo, miradi mitano imebainika kuwa na mapungufu na ilishauriwe kurekebishwa.
Bw. Makungu amesema kuwa mapungufu katika miradi miwili tayari yamefanyiwa kazi na Manispaa ya Kigamboni, huku mapungufu ya miradi mingine mitatu yakiendelea kufanyiwa kazi na ofisi ya TARURA-Temeke.
Amesema TAKUKURU inaendelea kuelimisha jamii kwa njia mbalimbali, zikiwemo kuimarisha klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari, na vyuo, kufanya mikutano ya hadhara na semina, kushiriki maonesho mbalimbali pamoja na kurusha vipindi vya televisheni na redio
“Tumejipanga kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa wananchi na wadau mbalimbali, hasa kuelekea uchaguzi wa viongozi wa kisiasa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu,” alisema Bw. Makungu.