Balozi wa Tanzania katika Ufalme wa Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi, tarehe 29 Mei, 2025, alifanya kikao na Watanzania wanaoishi nchini humo katika viwanja vya ofisi za ubalozi jijini Stockhom.
Katika kikao hicho kilicholenga kufahamiana na kujadiliana kuhusu masuala ya Diaspora, Mhe. Balozi Matinyi alielezea tafsiri ya neno “diaspora” kwa mujibu wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, toleo la mwaka 2024, iliyozinduliwa tarehe 19 Mei, 2025, jijini Dar es Salaam na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Balozi alieleza kuwa sera hii inawatambua Diaspora kuwa ni raia wa Tanzania wanaoishi nje (Citizen Diaspora) na raia wa nchi zingine wenye asili ya Tanzania (Non-Citizen Diaspora).
Mhe. Balozi Matinyi aliwaeleza Watanzania hao waliotoka miji mbalimbali ya Uswidi, kwamba sera hiyo imetambua ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya nchi yetu huku akirejea wito wa Mhe. Rais Dkt. Samia wa kuwataka Diaspora wawekeze nchini ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Akiinukuu hotuba ya bajeti bungeni ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, Mhe. Balozi Matinyi aliwaambia kwamba kwa mwaka 2024 Diaspora wa Tanzania waliwekeza fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.5 katika mfuko wa UTT-AMIS na shilingi bilioni 9.28 kwenye sekta ya milki kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na sekta binafsi.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Balozi Matinyi aliwataka wajenge umoja na ushirikiano kama alama kuu za Watanzania popote walipo duniani na kupigania maslahi ya nchi yao wakati wote.