Na Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema ili kutimiza malengo ya Milenia ya mageuzi ya Teknolojia yaliyopo duniani Tanzania imejipanga na iko tayari kushiriki katika uchumi wa kidijitali.
Hayo amezungumza leo Mei 30 jijini Dar es Salaam wakati akimuwakilisha Naibu waziri mkuu na waziri wa Nishati Dk Doto Biteko kwenye ufunguzi Mkutano Mkuu wa 14 wa Africa wa Utawala wa Mtandao, (AfIGF), ulioudhuriwa na wadau mbalimbali wa Afrika na nje ya Afrika.
Amesema serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya mageuzi mbalimbali ya kidigitali ikiwemo kuanzisha masomo ya ubunifu kuanzia shule za elimu ya awali hadi elimu ya juu ikiwa na lengo la kuchochea mageuzi ya kidigitali.
“kwasasa mtandao ni muhimu katika utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo maji, kwani, nishati ya umeme na nyinginezo, huvyo serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika mageuzi hayo”,amesema.
Amesema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha na kuboresha mazingira ya matumizi ya digitali ili kufikia lengo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa AflGF MAG, Alhagie Mbow, ameipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huo muhimu katika mageuzi ya Kidigitali Africa, ambao ni chachu kubwa ya mataifa hayo kukuza uchumi wake.
“Napenda kuipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huu mkubwa na nimatumaini yetu mijadala mbalimbali itakayojadiliwa hapa itakuja na mawazo chanya ya kuboresha na kupelekea kukuza uchumi katika nchi zetu”,Amesema.
Naye,Mwakilishi wa UNESCO, nchini, Michael Toto ameipongeza Tanzania kwa mkutano huo, huku akipongeza namna ambavyo wanaendeleza uchumi wa kidijitali.