Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Jerome Materu akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kongamano la afya na usalama mahali pa kazi lililofanyika leo Mei 29, 2025, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam.
Rasi wa Ndaki ya Tiba MUHAS Prof. Enica Richard akizungumza kwenye Kongamano la afya na usalama mahali pa kazi lililofanyika leo Mei 29, 2025, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Chuo Kikuu cha MUHAS Dk. Israel Nyarubeli akizungumza jambo kwenye Kongamano la afya na usalama mahali pa kazi lililofanyika leo Mei 29, 2025, MUHAS, Dar es Salaam.
Mtafiti wa masuala ya afya na usalama mahali pa kazi kutoka Chuo kikuu cha Afya kishiriki cha Muhimbili (MUHAS) Profesa Simon Mamuya akizungumza jambo kwenye Kongamano la afya na usalama mahali pa kazi lililofanyika leo Mei 29, 2025, Chuo kikuu cha MUHAS.
Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Joseph Kilago akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kongamano la afya na usalama mahali pa kazi lililofanyika leo Mei 29, 2025, Chuo kikuu MUHAS.
Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Jerome Materu akito tuzo ya heshima kwa ajili ya kutambua mchango wa watatifi katika afya na salama mahali pa Kazii
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya afya na usalama kazini wamewataka Watanzania, hususan wanaofanya kazi katika sekta zisizo rasmi, kuzingatia usalama wao wanapotekeleza majukumu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kazini.
Akizungumza wakati akifungua Kongamano la Afya na Usalama Mahali pa Kazi lililofanyika leo Mei 29, 2025 katika Chuo Kikuu cha MUHAS), Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Jerome Materu, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama kwa wafanyakazi wote, ikiwa ni sehemu ya kujenga Taifa lenye uchumi imara na wananchi wenye afya njema.
“Suala la elimu kuhusu vihatarishi kazini ni la msingi. Tafiti zinaonesha kuwa athari za kukosa usalama kazini ni pamoja na kupoteza mali, kupata magonjwa na hata vifo,” amesema Bw. Materu.
Ameongeza kuwa ajali mahali pa kazi huathiri kwa kiasi kikubwa mtu binafsi, familia na taasisi kwa ujumla. “Inapotokea ajali, mfanyakazi hupoteza kipato na afya, huku mwajiri akilazimika kutumia muda na rasilimali kuripoti tukio kwa vyombo vya sheria, jambo linaloweza kusababisha adhabu au faini,” amesema.
Kwa mujibu wa Bw. Materu, OSHA inaendelea kutoa elimu na vifaa vya usalama bila malipo kwa sekta zisizo rasmi kama hatua ya kuwawezesha kukua kiuchumi, huku wakilinda afya zao. Amewataka wadau katika sekta hiyo kujisajili OSHA ili waweze kupata ulinzi dhidi ya hatari zitokanazo na mazingira ya kazi.
Kwa upande wake, Mtafiti wa Masuala ya Afya na Usalama kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Simon Mamuya, amesema kuwa utafiti wao umebaini kuwa watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya kutumia vifaa hatarishi kazini.
“Sisi kama waelimishaji tunahitaji kuwafikia wananchi kwa wingi. Wakulima wengi, kwa mfano, hawajui madhara ya viuatilifu vinapoingia mwilini,” amesema Prof. Mamuya.
Ameongeza kuwa wachimbaji wadogo, hususan maeneo kama Mererani Mkoani Arusha, hawana elimu ya kutosha kuhusu madhara ya hewa chafu migodini, hali inayosababisha vifo vya vijana na watoto wanaojihusisha na kazi hizo.
Prof. Mamuya amesisitiza haja ya wataalamu na watunga sera, kukaa pamoja ili kuweka mikakati ya kuelimisha jamii na kudhibiti matumizi hatarishi ya viuatilifu na vifaa vya kazi.
Naye Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Bw. Joseph Kilago, amesema kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika afya na usalama kazini ili kupunguza mzigo wa magonjwa yanayotokana na mazingira ya kazi kwa mfumo wa utoaji huduma za afya.
“Msingi wa usalama kazini unaanza na mtu binafsi. Kila mtu anapaswa kuhakikisha usalama wake kulingana na mazingira ya kazi anayofanya,” amesema Bw. Kilago.
Amebainisha kuwa kazi ya serikali ni kutoa miongozo na kuhakikisha utekelezaji wake kulingana na mahitaji ya sekta husika kwa lengo la kuongeza tija kitaifa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kutoka MUHAS, Dkt. Israel Nyarubeli, amesema kuwa kongamano hilo lina tija kubwa kwa wataalamu na wadau wa sekta ya afya na usalama kazini.
“Huu ni mkutano unaowakutanisha watafiti, walimu, na wadau mbalimbali kwa ajili ya kushirikiana maarifa, kusherehekea mafanikio na kujadili changamoto zinazokumba maeneo ya kazi,” amesema Dkt. Nyarubeli.
Dkt. Nyarubeli ameeleza kuwa kongamano hilo, pia limetambua mchango wa waasisi wa taaluma hiyo, ikiwa ni pamoja na kutolewa tuzo maalum kwa Prof. Simon Mamuya kwa mchango wake mkubwa.
Aidha, sehemu ya pili ya kongamano hilo imehusu mijadala ya kisayansi, mijadala ya kisera na uwasilishaji wa tafiti zinazolenga kutafuta kinga dhidi ya ajali na madhara yatokanayo na kazi.
Kwa ujumla, wataalamu wametoa rai kwa jamii na taasisi kuwekeza katika elimu na mbinu za kuimarisha usalama mahali pa kazi ili kulinda rasilimali watu, kuongeza ufanisi na kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.