Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imesema imelipokea na italifanyia kazi ombi la wanaharakati wa haki ya afya ya uzazi wanaotaka kufanyike mabadiliko ya sheria kuhusu utoaji wa mimba zisizotarajiwa.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Winfrida Koroso, ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam Juni 30, 2025, wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Kukuza Afya ya Uzazi na Haki za Afya ya Uzazi kwa Wasichana Balehe na Wanawake wa Umri wa Kuzaa.
“Kuhusu mikakati ya uhamasishaji wa mabadiliko ya sheria na uchechemuzi unaoendelea katika eneo hili, niwahakikishie kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kama chombo kilichoundwa kisheria kwa nia ya kufanya utafiti na tathmini ya utekelezaji wa sheria mbalimbali, inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maslahi mapana ya Watanzania,” amesema Jaji Koroso.
Ameongeza kuwa Tume itayafanyia kazi majadiliano ya warsha hiyo, na itaendelea kuunga mkono jitihada zote zinazolenga kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi, hasa kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18.
Ameeleza kuwa kwa zaidi ya miaka 25, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kimekuwa mstari wa mbele katika kufanya uchechemuzi, kuendesha kesi za kimkakati na kufanya tafiti kuhusu masuala ya wanawake na watoto, kwa lengo la kuendeleza haki za uzazi.
Aidha, Jaji Koroso ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana katika kulinda haki za uzazi na kuhakikisha sheria zinakuwa rafiki ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Alisema juhudi hizo zinalenga kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDG) ifikapo mwaka 2030, ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000, vifo vya watoto hadi 25 kwa kila vizazi hai 1,000, na vifo vya watoto wachanga hadi 12 kwa kila vizazi hai 1,000.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2006 hadi kufikia 104 kwa mwaka 2022 — jambo ambalo limetajwa kuwa ni matokeo ya mikakati iliyopo na sheria zinazoruhusu upatikanaji wa huduma bora.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Elias Kweyamba, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ifakara, amesema utoaji mimba usiosalama—unaofanywa na watu wasiokuwa wataalamu kwa njia zisizokubalika—unasababisha madhara makubwa ya kiafya kama ugumba, kutokwa damu nyingi, fistula na maambukizi ya magonjwa ikiwemo UKIMWI.
Dkt. Kweyamba amesema takribani wanawake 400,000 hutolewa mimba kila mwaka nchini Tanzania, hali inayochangiwa na mimba zisizotarajiwa, hali ngumu ya kiuchumi, na elimu ndogo kuhusu uzazi wa mpango.
“Watu wanapata mimba wakiwa masomoni na hulazimika kutoa mimba ili wasitishwe ndoto zao. Lakini pia matumizi ya uzazi wa mpango yako chini kutokana na changamoto za upatikanaji na uelewa,” amesema.
Ameeleza kuwa wengi wangependa kutoa mimba kwa njia salama lakini sheria zilizopo haziwaruhusu isipokuwa tu pale ambapo maisha ya mama yako hatarini, hali inayowalazimu watu kutoa mimba kwa siri katika mazingira hatarishi.
“Kwa sababu sheria hairuhusu, watu wanalazimika kwenda mafichoni. Hili ni janga linalohitaji ushirikiano kati ya serikali na wadau kuhakikisha mimba zinazuiwa mapema au zikitolewa, basi iwe kwa usalama,” amesema Dkt. Kweyamba, na kufichua kuwa kesi za ubakaji ziliorodheshwa na Polisi mwaka 2023 zilikuwa 8,639.
Kwa upande wake, Wakili Peter Majanjalo amesema Tanzania imesaini Mkataba wa Maputo unaoruhusu utoaji wa mimba kwa wahanga wa ubakaji, ndoa za maharimu, au pale ambapo ujauzito unahatarisha afya ya mwili au akili ya mwanamke. Hata hivyo, vifungu vya sheria vya Kanuni ya Adhabu (CPA) yaani kifungu cha 150, 151 na 152 bado vinazuia utoaji mimba kwa mazingira yoyote yale.
“Kwa sasa, mtu yeyote atakayesaidia kutoa mimba anaweza kuhukumiwa miaka 14 jela, mwanamke mwenyewe miaka saba, na atakayetoa dawa au vifaa miaka mitatu. Hii inawazuia hata watoa huduma waliobobea kusaidia wahitaji. Sheria ikibadilishwa, huduma zitatolewa kwa usalama na kuepuka athari zinazotokana na utoaji mimba usio salama,” amesema Wakili Majanjalo.
