Na. Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kupitia kikosi cha Usalama barabarani kimefanya ukaguzi maalumu wa mabasi ya abiria kwa ajili ya kudhibiti ajali kutokana na uwepo wa ongezeko kubwa la abiria kufuatia kuanza kufungwa kwa Shule.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed leo wakati akizungumza na madereva katika Stendi kuu ya mabasi Mkoani humo amesema msimu huu wanafunzi wengi wanasafiri kuelekea mikoani hivyo kunasababisha kuwepo kwa ongezeko la abiria.
SSP Zauda amebainisha kuwa kutokana na ongezeko hilo la abiria pamoja na magari binafsi, madereva wanapaswa kuendesha magari yao kwa tahadhari kubwa huku wakizingatia na kufuata sheria za usalama barabarani wakati wote ili kuepuka ajali.
Pia amewataka madereva hao pindi wanapopata changamoto barabarani ikiwepo kuharibika kwa magari yao kuhakikisha wanayaondoa na kuyaweka pembeni au kuweka alama ambazo zitasadia watumiaji wengine wa barabara kuona.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za abiria Kanda ya Kaskazini Bw. Godwin Mpinga amesema baadhi ya mabasi sio wa wakweli kuhusu safari zao hivyo akatoa wito kwa abiria kuhakikisha pindi wanapotaka kusafiri kufika katika Ofisi husika ya mabasi kwa ajili ya kupatiwa tiketi nasiyo sehemu nyingine ili kuepusha usumbufu.
Naye wakala wa mabasi Bw. Rashid Mohamed amesema katika ukaguzi huo wamepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kueleza changamoto zao ambazo zinawakabiliMbali na kushukuru kwa elimu ambayo wameipata toka kwa mkuu wa usalama barabarani.