Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi amesema Sekretarieti ya Maadili itaendeleza ushirikiano na vyombo vya Habari nchini na kuvitaka kuendelea kuandika habari zinazoeleza umuhimu wa Maadili kwa Viongozi wa Umma.
Jaji Mwangesi amesema hayo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Wahariri nchini wenye lengo la kutoa elimu na kuendeleza ushirikiano na Chombo hicho katika kueleza kazi, majukumu na mafanikio ya Sekretarieti ya Maadili.
Mkutano huo ulifanyika tarehe 30 Mei, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya PEACOCK jijini Dar-es-Salaam.
‘’Sekretarieti ya Maadili inatambua juhudi kubwa za vyombo vya Habari katika kukuza Maadili ya Viongozi wa Umma nchini kwa kutumia kalamu zenu katika kuelimisha, kuhabarisha, kuburudisha pamoja na kukosoa kuhusu dhana ya Uadilifu na uwajibikaji kwa viongozi wa umma,’’alisema Jaji Mwangesi.
“Ndugu zangu Wahariri ni wazi zipo taarifa nyingi tunazozifanyia kazi kuhusu Viongozi wa Umma, ambazo bila jitihada zenu tusingezijua hii inaonyesha kuwa vyombo vya habari ni mdau na msaada mkubwa katika kukusanya taarifa muhimu na za ukweli zinazipa nguvu jamii kujua hali ya uadilifu nchini”. Aliongeza Mwangesi.
Aidha, Mwangesi amewaomba Wahariri kuendeleza weledi na kutumia taaluma zao kwa kutoa taarifa sahihi na zenye ulinganifu ambazo zitawasaidia wananchi kuchagua Viongozi waadilifu katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu baadae mwaka huu.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi Ukuzaji wa Maadili, Bw. Fabian Pokela ametumia fursa hiyo kutoa elimu ya majukumu na kazi zinazofanywa na Sekretarieti ya Maadili na kutoa wito kwa Wahariri kusaidia kutoa elimu ya Maadili kwa jamii.
Nao, Wahariri wamemuomba Kamishna wa Maadili kuendelea kutoa elimu kwa umma ili jamii iweze kufahamu majukumu na kazi zinazofanyika na Sekretarieti ya Maadili.
Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Bw. Salim Salim ameishukuru Sekretarieti ya Maadili kwa kuwaongezea uelewa wajumbe wake kuhusu masuala mbalimbali ya Maadili kwa Viongozi wa Umma yatakayo wasaidia kutekeleza vizuri majukumu yao.