Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Missaile Musa akipata maelezo kutoka kwa Afisa Bima Tira kanda ya kaskazini Arusha,Goodluck Massawe wakati alipotembelea kwenye banda lao jijini Arusha .

Mrajisi msaidizi vyama vya ushirika ,Josephat Kisamalala akizungumza kwenye jukwaa hilo jijini Arusha.

Mwenyekiti wa jukwaa la maendeleo ya ushirika mkoa wa Arusha ,Maria Maembe akizungumza kwenye jukwaa hilo jijini Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
.WAAJIRI nchini wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kuchelewesha michango ya wanachama wao badala yake wapeleke kwa wakati kwenye vyama vya ushirika .
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, Missaile Musa wakati akifungua jukwaa la saba la wadau wa maendeleo ya ushirika mkoa wa Arusha lililofanyika jijini Arusha .
Musa amesema kuwa, kumekuwepo na changamoto kubwa ya waajiri kuchelewesha michango ya wanachama na kutoipeleka kwenye vyama vya ushirika kwa wakati jambo ambalo linakuwa ni changamoto wakati wa kufuatilia michango yao.
“Nawaombeni sana muwe mnawasilisha michango hiyo kwa wakati ili kuepuka migogoro mbalimbali inayotokana na uchelewaji na kwa kufanya hivyo wataweza kupata haki zao za msingi.”amesema .
Aidha amewataka pia wanachama hao kurejesha kwa wakati mikopo pindi wanapokopa ili kuwezesha na wengine kuweza kupata mikopo hiyo.
Ameongeza kuwa, uwepo wa vyama hivyo unasaidia sana wananchi kuimarika kiuchumi na kusaidia kuwepo kwa nidhamu ua kifedha kwa wanachama wake.
Aidha amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kushirikiana pamoja katika kuimarisha ushirika kwani wananchi wanapojiunga wanapata fursa ya kunufaika na maswala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa jukwaa la maendeleo ya ushirika mkoa wa Arusha ,Maria Maembe amesema kuwa mchango wa sekta ya ushirika nchini ni mkubwa sana kwani wamekuwa wakitoa mikopo ambayo inawasaidia wananchi katika.maswala mbalimbali.
Aidha amesema kuwa, kila mmoja anaruhusiwa kujiunga na kuweza kuweka akiba na kukubaliana na masharti yaliyowekwa kwani wamekuwa wakitoa mikopo ya masharti nafuu ambayo inasaidia wanachama wake kuweza kujikimu kiuchumi.
Naye Mrajisi msaidizi vyama vya ushirika ,Josephat Kisamalala amesema kuwa ,Ushirika unaendelea kukua kwa kiwango kikubwa na watu wanaendelea kuwa na imani na chama hicho kutokana na namna wanavyotoa huduma zao kwa kuwafikia wanachama wake kwa kutoa mikopo kwa wakati na kwa muda wote wanaohitaji.
Aidha alivitaka vyama hivyo kuhakikisha vinatumia mfumo wa Tehama katika kufanya shughuli zao kwani ni lazima wafike mahali sasa wajiendeshe kidigitali .
Kisamalala amewataka viongozi wa vyama hivyo kuhakikisha wanaongeza nguvu zaidi katika kutoa elimu juu ya vyama hivyo na umuhimu wa kujiunga ili wananchi wajiunge kwa wingi na kuweza kupata wanachama wengi zaidi kwani waliopo bado ni wachache sana .
“Naombeni sana viongozi muone namna mtajipanga kwenda kuhamasisha soko ili tupate wachama wengi zaidi na chama kizidi kukua kikubwa muendelee kutoa elimu ili watu wahamasike kujiunga na hatimaye kupata wanachama wengi.”amesema Kisamalala.