Na Prisca Libaga Same
Wananchi wa Kata ya Tae, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) pamoja na Serikali ya Wilaya ya Same tarehe 30.05.2025 wameshiriki zoezi la kung’oa visiki vya mimea ya dawa za kulevya aina ya mirungi iliyopandwa katika Kijiji cha Heikonti kilichopo ndani ya Kata ya Tae wilayani Same.
Hamasa ya wananchi wa kijiji hicho kwa hiari wameamua kung’oa visiki vya mirungi kufuatia elimu waliyoipata kutoka katika mamlaka za Serikali ikiwemo DCEA katika kutafuta suluhu ya kukabiliana na kilimo cha dawa za kulevya aina ya mirungi ambapo tayari Serikali imeshapata mazao mbadala zaidi ya nane kwa Wanakijiji wa Kata za Tae, Vudee na maeneo mengine ambayo hapo awali yalishamiri kwa kilimo cha mirungi.
Sehemu ya visiki vya mirungi vilivyong’olewa kwa hiari na wananchi katika Kijiji hicho inatokana na operesheni kubwa ya uteketezaji wa mashamba ya mirungi iliyofanyika Mwezi Machi 2025 chini ya usimamizi wa Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo katika Vijiji na Vitongoji vilivyopo ndani ya Kata za Tae na Vudee katika Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Zoezi la wananchi la kuamua kung’oa visiki kwa hiari katika Kata za Tae na Vudee na maeneo mengine kwa kushirikiana na DCEA pamoja na Serikali ya wilaya ya Same ni endelevu.
Aidha, Maafisa wa DCEA kwa kushirikiana na TAKUKURU wametoa elimu kinga dhidi ya dawa za kulevya pamoja na kupinga rushwa kwa wanafunzi zaidi ya 350 wa Shule ya Sekondari ya Tae iliyopo Kata ya Tae katika Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Pamoja na elimu hiyo waliyoipata wanafunzi hao lakini pia walihamasishwa kushirikiana na DCEA katika kuwafichua wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga simu ya bure 119.






