Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga
Kwa mwaka huu wa 2025, moja ya tukio kubwa kabisa katika kalenda ya nchi yetu ni uwepo wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2025.
Hili ni tukio la kidemokrasia na la kikatiba ambapo Watanzania wanapata fursa ya kutimiza haki yao ya kisheria na kikatiba ya kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo yaani 2025-2030.
Kwa kuzingatia kuwa lengo la kwanza la chama chochote cha kiasi ni kushinda uchaguzi ili kushika dola, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wake kimejizatiti si tu kushiriki katika Uchaguzi Mkuu lakini pia kushinda kwa kishindo kikubwa.
Pamoja na sera nzuri ambazo CCM inazo, lakini uwekezaji mkubwa umefanyika wa kusajili wanachama kwa njia ya kieletroniki ili kuwa na uhakika wa ushindi ikizingatiwa watu ni mtaji muhimu wa kufanikisha ushindi.
Mei 29, 2025, jijini Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema chama hicho kina jumla la wanachama 13,000,670 (Milioni Kumi na Tatu Mia Sita na Sabini) kutoka kila kona ya nchi huku akibainisha idadi hiyo ni ishara ya wananchi kuwa na imani na chama hicho katika kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.
Wanachama Milioni 13 ni idadi kubwa sana ambapo hamasa ikiendelea kuwekwa ili kujitokeza kwa wingi kupiga kura, itakuwa ni mtaji mzuri kuelekea ushindi wa kishindo.
Sambamba na hilo, Dk. Samia Suluhu Hassan ametoka wito kwa vijana kujiunga na chama hiki ili wawe sehemu ya maendeleo kwa wananchi. “CCM ni chama Cha watu wote, vijana wanapaswa kukiona kama sehemu yao.Tunawakaribisha wajiunge ili washiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya Taifa,” asema Dk. Samia.
Sambamba na hilo, Mei 30, 2025, CCM ilizindua Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030 ambapo vipaumbele tisa viliwekwa wazi ambavyo vitaelezwa kwa wananchi ili kuomba ridhaa ya kuwaongoza.
Pamoja na wingi wa wanachama hao ambao CCM inao, bado juhudi zaidi zinahitajika katika kuhakikisha inapitisha wagombea bora wanaokubalika ndani na nje ya chama ili waweze kukipa chama ushindi. Pia, kuwashawishi wanachama wa vyama vingine na wananchi wasio na vyama kukichagua chama hicho katika Uchaguzi Mkuu.
Maoni: 0620 800 462.