Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mwanasiasa kijana kutoka Kata ya Mhezi, Ndg. Anthony Ishika Mghamba, ambaye ni Naibu Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii WA Baraza Kivuli la ACT wazalendo amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa na chama cha ACT-Wazalendo kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Same Magharibi katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Mghamba alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa Same Magharibi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi bila kujali itikadi za vyama wala dini.
“Sasa imefika mwisho, hatuko tayari kudhulumiwa na CCM maendeleo tunayostahili kama walipa kodi. Tukaungane kwa pamoja kwenye boksi la kura kutetea #SameYaWote yenye #MaslahiYaWote,” alisema Mghamba.
Mghamba alieleza kuwa ubunge si nafasi binafsi bali ni dhamana ya wananchi wanaochagua, na kwamba iwapo atateuliwa na kuchaguliwa, atahakikisha Same Magharibi inapata maendeleo ya haraka na huduma bora za kijamii.
Alitaja changamoto kadhaa zinazolikabili jimbo hilo zikiwemo gharama kubwa za maisha, ukosefu wa ajira, huduma duni za afya, elimu, miundombinu mibovu ya barabara, uhaba wa maji, pamoja na mazingira duni ya kilimo, ufugaji na biashara.
“Nina dhamira ya dhati ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii. ‘Same ya Wote’ ni wito wangu kwa kila mwananchi wa Same ili kuungana kupigania serikali inayowajibika na kufanikisha huduma bora kwa wote,” aliongeza.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa muda wa kampeni bado haujafika kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi, hivyo kwa sasa alikuwa akitangaza nia tu ya kugombea.
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uteuzi ndani ya vyama vya siasa unaendelea nchini kote, huku wagombea wakitakiwa kuzingatia maadili ya kisiasa na masharti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).