Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imerekodi ongezeko la asilimia 40 katika makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi ndani ya kipindi cha miezi 11, ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita.
Akizungumza katika kikao na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu, Juni 2, 2025, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema serikali imekusanya Sh884.7 bilioni kuanzia Julai 2024 hadi Mei 2025.
Hili ni ongezeko kubwa la mapato yanayokusanywa kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, ikilinganishwa na Sh633.3 bilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2023/24.
Pia hii inaonyesha ongezeko la asilimia 15.3 ikilinganishwa na jumla ya makusanyo ya mwaka mzima ya Sh767 bilioni katika mwaka wa fedha uliopita.
Bw. Mchechu alisema ukuaji huo wa mapato umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika Mashirika ya umma na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.
“Ofisi imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Mpango na Bajeti (PlanRep) na Mifumo ya ERMS na e-Watumishi pamoja na kufanya maboresho ya Mfumo wa MUSE ambao unawezesha kupata taarifa halisi za matumizi katika Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za Umma,” alisema Bw. Mchechu
Alisema maboresho hayo sasa yamefanya mifumo kubadilishana taarifa ipasavyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuona mifumo inasomana.
Akivitaja vyanzo vikuu vya mapato kwa mwaka huu amesema ni gawio ambalo limechangia asilimia 63.9 ya mapato yote, huku michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ikichangia asilimia 29.7.
Aidha, mapato mengineyo yaliyojumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yamechangia asilimia 6.4 ya mapato yote.
Mbali na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato, pia uwekezaji katika kuimarisha utendaji wa watumishi wao kupitia viashiria muhimu vya utendaji (KPIs) umetajwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kupitia KPIs, Ofisi hiyo imeweza kufanya tathmini za utendaji wa Bodi, ili taasisi ziwe na matokeo yanayopimika kwa uwazi na uwajibikaji.
“Hili limeenda sambamba na kuwajengea uwezo Viongozi wetu ambapo jumla ya Watendaji Wakuu 111 walishiriki mafunzo elekezi ya uongozi na usimamizi (CEO Induction) mwaka huu, ili kuimarisha utawala bora na uhusiano wa kiutendaji,” alisema Bw. Mchechu.
Hata hivyo, ili kuongeza ufanisi zaidi na ukusanyaji wa mapato, Serikali iliongeza uwekezaji wake katika mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
Sasa thamani ya uwekezaji wake imetoka Sh75.79 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh86.29 trilion imwaka 2023/24
“Pia tumeweza kuhamasisha uwajibikaji katika kampuni hizi kupitia Mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi wanaoiwakilisha Serikali katika kampuni zenye hisa chache uliowaleta washiriki 125 na kuzindua Mwongozo Ulioboreshwa wa Wakurugenzi,” alisema Bw. Mchechu.
Kwa mujibu wake, hilo limeenda sambamba na kupitia Mikataba na Kuimarisha Usimamizi wa Hisa huku ikiongeza ushiriki wake katika kampuni muhimu kwenye sekta za benki, viwanda na madini kupitia maboresho ya mikataba ya wanahisa na miundo ya usimamizi.
Kuhusu siku ya gawio
Akizungumzia siku ya gawio 2025, Bw. Mchechu alisema inatarajiwa kufanyika Juni 10, mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema katika siku hiyo, taasisi na mashirika ya umma yatamkabidhi rasmi Mhe. Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan, michango na gawio kwa Serikali.
“Tukio hili ni muhimu sana si tu kama alama ya uwajibikaji, bali pia kama chombo cha kutathmini utendaji wa mashirika na taasisi za umma kwa mujibu wa malengo ya Taifa,” alisema Bw. Mchechu.
Amesema Siku ya Gawio imekuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi na mafanikio yanayooneka leo kwani tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu wa wazi na wenye uwajibikaji, kumekuwa na ongezeko la mashirika yanayotoa gawio, pamoja na kuboreshwa kwa utendaji wao kwa ujumla.
“Hii ni ishara kuwa pale ambapo taasisi za umma zinasimamiwa kwa weledi, mafanikio ya kweli yanawezekana,” alihitimisha Bw. Mchechu.