OR-TAMISEMI
Ngoma za asili, kwaya na Muziki wa Kizazi kipya (Bongo Flavor) ni sehemu ya fani ambazo zimekuwa zikishindaniwa katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa shule za Msingi na Sekondari (UMITASHUMTA & UMISSETA).
Mratibu wa michezo- TAMISEMI, Yusuph Singo amesema kupitia sanaa, wanafunzi wanapata nafasi ya kuonesha vipaji vyao katika kucheza ngoma zenye asili ya makabila ya mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, kuimba nyimbo zenye ujumbe wa kizalendo na kuburudisha kupitia muziki wa kizazi kipya.
Mikoa inayoshiriki UMITASHUMTA & UMISSETA 2025 Mkoani Iringa inatarajiwa kuwa na uwakilishi wa vikundi vya ngoma, kwaya na waimbaji wa muziki wa kizazi kipya kwa ajili ya kushindana na kumpa mshindi wa mashindano ya mwaka huu.
Mashindano hayo yenye kauli mbiu isemayo “Viongozi bora ni msingi wa maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu” yataanza Mei 7 2025 na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Mjini Iringa tarehe 9 Mei 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa.
Ofisi ya Rais-TAMISEMI ndio mratibu na msimamizi wa UMITASHUMTA & UMISSETA 2025 ikishirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, na Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo.