Rais wa Jamhuri ya Kosovo, Mhe. Dkt. Vjosa Osmani Sadriu amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipomtembelea Ikulu jijini Prishtina, Kosovo tarehe 1 Juni 2025.
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Kosovo hususan katika maeneo ya kimkakati kama vile biashara, uwekezaji, kilimo na utalii.
Awali akizungumza, Mhe. Rais Sadriu amesema kuwa amefarijika kwa Tanzania kuitikia mwaliko wake wa kushiriki Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ambao yeye ni mmoja wa waanzilishi wake.
Ameongeza kusema kuwa, nchi yake inathamini ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili na kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kidiplomasia na ushirikiano wa uwili kwa maslahi mapana ya wananchi wa mataifa haya mawili.
Akizungumzia suala la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kosovo, Mhe. Rais Sadriu amesema nchi yake inaunga mkono pendekezo la kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika masuala ya Uchumi (Joint Economic Commission) na kwamba yupo tayari kutuma ujumbe wa wafanyabiashara kwenda Tanzania ili kuangalia fursa zilizopo nchini.
Kwa upande wake, Mhe. Waziri Kombo amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Kosovo na kuahidi kuendelea kushirikiana na nchi hiyo hususan katika kukuza biashara, uwekezaji na utalii ambapo alitumia pia nafasi hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Kosovo kuja nchini na kujionea fursa lukuki za biashara na uwekezaji zilizopo.
Tanzania inaweza kunufaika na fursa ya soko la Kosovo kwa kuuza bidhaa zake kama vile samaki na mazao mengine ya baharini, viungo vya chakula, ngozi na matunda.
Mhe. Waziri Kombo na ujumbe wake yupo nchini Kosovo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama utakaofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 3 Juni, 2025.