Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Rhobi Samuel amesema suala la utunzaji wa mazingira ni la kila mwana jamii hivyo kutoa wito kwa kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anapanda miti katika eneo lake.
Rhobi amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua utunzaji na usimamizi wa miti iliyopandwa katika baadhi ya shule za Sekondari katika Manispaa ya Musoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani.
“Tusisiburi kampeni za balozi wa mazingira ndipo tupande miti,kila mtu kwa nafasi yake na katika eneo lake anapaswa kupanda miti kwa wingi kadri awezavyo, hakika hili likifanyika tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari zake tayari tumeanza kuziona,” amesema
Amesema serikali imedhamiria kuongeza idadi ya watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2034 na kwamba dhamira hiyo inatakiwa kwenda sambamba na suala zima la uboreshaji wa mazingira ikiwepo upandaji wa miti.
“Wakati tunajipanga kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia lazima tuhakikishe mazingira yanakuwa salama, tunapanda miti na kuitunza kwani sote tunajua faida ya miti jwa ustawi wa mwanadamu hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kujua ana wajibika kwa kiasi kikubwa kulifanikisha hili,” amesema
Amesema mbali na upandaji miti watazania pia wanapaswa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali ikiwa ni pamoja na kilimo himilivu, matumizi sahihi ya vyanzo vya maji masuala ambayo ni sehemu ya mpango mkakati wa kukabiliana na mabadiliko hayo ya tabia nchi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Balozi wa mazingira nchini, Jairos Sinene amesema zaidi ya miti 45,000 imepandwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani Mara katika kipindi cha miaka minne iliyopita kupitia kampeni maalum aliyofanya.
Amesema kati ya miti hiyo iliyopandwa zaidi ya miti 35,000 imekuwa huku miti 10,000 ikishindwa kukua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuliwa na mifugo pamoja na kukosa utunzaji kutoka kwa taasisi husika.
“Hii miti 45,000 ni tofauti na ile iliyoelekezwa na serikali ambapo kila halmashauri inatakiwa kupanda miti 1.5 milioni kila mwaka,hii ni kampeni maalum ya kuhamasisha taasisi za umma kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira ili kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia kutokana na uharibifu wa mazingira ikiwepo ukataji wa miti,” amesema
Amesema ufuatiliaji na usimamizi imara umesababisha miti iliyopandwa katika kampeni hiyo kukua kwa zaidi ya asilimia 95 hivyo kutoa wito kwa wadau wengine kuhakikisha panakuwepo na ufuatiliaji baada ya upandaji miti.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwisenge,Theopista Mashauri amesema kupitia kampeni hiyo shule yake ilipanda miti 1,000 ambapo miti 968 imeweza kukua.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ufuatiliaji unaofanywa na uongozi wa shule mara kwa mara lengo likiwa ni kuifanya shule hiyo kuwa ya kijani.
“Tunalenga ‘kuikijanisha’ Mwisenge sasa ili kufikia lengo hili, yapo mambo kadhaa tuliyokubaliana ikiwa ni pamoja na kila mwanafunzi kukabidhiwa mti wake ambao anatakiwa kuutunza hadi atakapohitimu kidato cha nne,” amesema