WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuimarisha misingi ya utawala bora kwa watumishi wake kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara yanayolenga kuongeza uadilifu, uwajibikaji na kupambana na vitendo vya rushwa katika maeneo ya kazi.
Katika muendelezo wa juhudi hizo, leo Juni 3, 2025, TFS imekaribisha Maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa katika Shamba la Miti Sao Hill kwa ajili ya kutoa elimu kwa wahifadhi kuhusu namna ya kuepuka na kupambana na rushwa, sambamba na kuimarisha maadili ya utumishi wa umma.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Bw. Victor Swella, alisema elimu hiyo inalenga kuwakumbusha watumishi kuhusu wajibu wao kwa umma na kuhimiza matumizi sahihi ya madaraka waliyopewa ili kuimarisha uwajibikaji na kuondoa mianya ya rushwa.
“Kila mtumishi wa umma anapaswa kutumia madaraka aliyopewa kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria. Kutekeleza majukumu kwa uadilifu ni msingi wa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuendeleza misingi ya utawala bora mahali pa kazi,” alisema Swella.
Aliongeza kuwa vitendo vya rushwa huathiri siyo tu ufanisi wa taasisi, bali pia maisha ya watumishi binafsi na familia zao, hasa pale vinapozua mashtaka au adhabu za kisheria. Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kama vile kutunza siri za ofisi, kutoa huduma bila upendeleo, kutumia taarifa kwa usahihi, na kuwa waaminifu kwa mamlaka zao.
Akizungumza kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Peter Fitwangile aliwashukuru TAKUKURU kwa kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa watumishi wa TFS, akieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha utendaji kazi na kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa ipasavyo.
“TFS inaendelea kufanya maboresho ya kiutendaji kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ambayo inarahisisha utoaji wa huduma, kupunguza mianya ya rushwa, na kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali,” alisema Fitwangile.
Aliongeza kuwa mafunzo yanayotolewa yamekuwa yakisaidia sana watumishi kuelewa vizuri wajibu wao na namna bora ya kushughulikia changamoto za kiutumishi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Shamba la Miti Sao Hill, Bi. Felista Bayo, aliipongeza TAKUKURU kwa kuitikia wito wa kutoa mafunzo kwa watumishi, akisema elimu hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuwajenga watumishi kuwa waadilifu na kuepuka maamuzi yasiyo sahihi yanayoweza kuleta madhara kwa taasisi na jamii kwa ujumla.
“Elimu hii ni muhimu kwa wakati huu ambapo taasisi nyingi za umma zinapitia mabadiliko ya kiteknolojia. Ni lazima tuhakikishe kuwa pamoja na kutumia mifumo ya kisasa, maadili ya kazi na kanuni za utumishi wa umma vinafuatwa kikamilifu,” alisema Bayo.
TFS imeendelea kuwa kinara katika kusimamia misitu na kuendeleza sekta ya nyuki kwa kutumia mifumo ya kisasa, huku ikijikita katika kujenga utumishi wenye weledi, uwajibikaji na maadili kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za udhibiti na usimamizi nchini.
