WAZIRI MKUU MAJALIWA KUWEKA JIWE LA MSINGI JENGO LA VIWANGO HOUSE KESHO JUNI 04,2025 DODOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari Leo Juni 3,2025 katika Ukumbi wa TBS jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari Leo Juni 3,2025 katika Ukumbi wa TBS jijini Dodoma.
……
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la TBS (VIWANGO House) kesho Juni 04,2025 katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, ameyasema hayo leo Juni 03,2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa TBS jijini Dodoma.
.
Amesema jengo hilo mpaka hivi sasa limefikia asilimia 76 kwenye ujenzi, na ni jengo la kimkakati katika makao makuu ya nchi jijini Dodoma.
.
“Tunatarajia jengo hili litaendelea kuongeza thamani katika makao makuu ya nchi, lakini pia litaongeza thamani kwa watanzania ambao tunawahudumia” alisema Dkt. Katunzi.
.
Dkt. Katunzi amesema jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu ambazo zitakuwa na maabara, ambapo katika maabara hizo kutakuwa na maabara ya chakula, maabara ya kemia,maabara ya nguo (Textiles materials) na maabara ya metrolojia (huduma za ugenzi)
.
“Maabara hizi zikiwepo Jijini Dodoma zitasaidia kuleta ufanisi katika kazi zetu na wananchi tunaohudumia, kwa sasa TBS Maabara zetu zote zipo Dar Es salaam, sampuli zote tunazozikusanya katika nchi hii ili kufanya maamuzi ya ubora na usalama lazima zipelekwe Dar” alisema Dkt. Katunzi.
.
Aidha, Dkt. Katunzi amesema gharama za ujenzi wa jengo hilo ni shilingi Bilioni 25 za kitanzania.
.
Sambamba na hilo,Dkt. Katunzi amesema Shirika linaendelea kuwekeza na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wake ambapo wanatarajia pia kuanza ujenzi wa jengo la kanda ya kaskazini mkoani Arusha, na ujenzi huo utaanza ndani ya Mwaka wa Fedha ujao 2025/26.
.
“Tumeshaanza ujenzi kanda ya ziwa mkoani Mwanza, jengo hilo lina ghorofa tano (5) na ujenzi umefikia asilimia 30” amesema Dkt. Katunzi.