Na John Bukuku – Mahakama ya Rufani, Dodoma
Dodoma, Juni 4, 2025,
Mahakama ya Rufani ya Tanzania leo imetoa uamuzi wake katika Rufaa Namba 658 ya mwaka 2023, iliyowasilishwa na Mwananchi Communications Ltd pamoja na Mhariri wa The Citizen Newspaper, dhidi ya Nehemia Kyando Mchechu, na kutupilia mbali maombi hayo kwa kukubaliana na maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyotolewa tarehe 3 Machi 2023 mbele ya Jaji Mgonya.
Katika uamuzi huo uliotolewa mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, mahakama hiyo ilipitia hoja kuu tatu zilizowasilishwa katika rufaa hiyo. Hoja hizo ni pamoja na:
- Iwapo Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo,
- Iwapo mdai (Mchechu) aliweza kuthibitisha madai yake ya kudhalilishwa,
- Iwapo Mahakama Kuu ilitumia utaratibu sahihi kutoa nafuu na fidia zilizotolewa.
Majaji wa Mahakama ya Rufani walikubaliana na hoja zilizowasilishwa na wakili wa upande wa mjibu rufani, Wakili Aliko Harry Mwamanenge, na kueleza kuwa:
- Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo halali wa kusikiliza shauri hilo;
- Mdai (Mchechu) aliweza kuwasilisha ushahidi thabiti kuthibitisha kuwa alidhalilishwa;
- Mahakama Kuu ilifuata misingi sahihi ya kisheria katika kutoa nafuu zilizotolewa katika hukumu yake.
Kwa mantiki hiyo, Mahakama ya Rufani haikuona sababu yoyote ya kubatilisha au kurekebisha maamuzi ya Mahakama Kuu, hivyo ikayathibitisha maamuzi hayo kama yalivyotolewa.
Katika uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu, Mwananchi Communications Ltd pamoja na Mhariri wa The Citizen Newspaper walikutwa na hatia ya kuchapisha taarifa zilizomdhalilisha Nehemia Kyando Mchechu, na mahakama ikaamuru walipe fidia pamoja na gharama nyingine kama ilivyoainishwa katika hukumu ya Machi 3, 2023.
Kwa hatua hii ya Mahakama ya Rufani, kesi hiyo sasa imefungwa rasmi huku maamuzi ya Mahakama Kuu yakiendelea kusimama kama yalivyo
Rufaa hiyo ilisikikizwa chini ya majaji watatu ambao ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Rehema Kerefu, Jaji Omar Othman Makungu na Jaji Dkt.Benhajj Masoud