Mhe. Simon Makoye Mayengo akitangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Na Kadama Malunde -Malunde 1 blog
Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Mhe. Simon Makoye Mayengo ametangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Mayengo ametangaza uamuzi huo leo Juni 4,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuandika na kukabidhi barua ya kupisha vikao vya uteuzi wa wagombea ndani ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu 2025.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano maalum wa CCM uliofanyika Dodoma Mei 29 na 30,2025 alitoa maelekezo viongozi wote wenye nyadhifa za uteuzi, kamati za siasa, kamati za utekelezaji wilaya pamoja na mkoa kwenye Chama Cha Mapinduzi wanatakiwa kuandika barua kupisha uteuzi kwa ajili ya wagombea ambao utafanyika Mwezi Julai baada ya mabaraza ya madiwani pamoja na Bunge kuvunjwa”,ameeleza Mayengo.
Mayengo amesema kuwa yeye kama Mjumbe wa kamati ya siasa CCM Mkoa wa Shinyanga leo amepeleka barua kwa katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwani na yeye ni mtia nia katika jimbo la Ushetu ambapo ndiyo amezaliwa Ushetu na anaishi Ushetu.
“Nimeamua kutangaza nia kugombea ubunge Jimbo la Ushetu kwa sababu jimbo la Ushetu lilikuwa na Hayati Elias Kwandikwa kati ya 2015 hadi 2021 alipofariki dunia ndipo tukampata Mhe. Emmanuel Cherehani ambaye naye amefanya kazi yake.
“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi Mkuu na mimi kama mwana Ushetu leo Juni 4,2025 natamka rasmi kwamba nimetia nia Ushetu, natangaza rasmi kwamba naenda kugombea Jimbo la Ushetu. Tunaenda kuikomba Ushetu kwa sababu Mbunge aliyepo tunaona hatoshi”,amesema Mayengo.
“Kwa hiyo tumeamua kuikomboa Ushetu, tumeamua kwenda kuitengeneza Ushetu mpya kama tuliyokuwa nayo zamani kwani katika miaka mitatu tumeona Ushetu haitendewi haki, tunataka mwakilishi wa kweli, sisi tunataka maendeleo, na maendeleo hayaendi. Tunataka Ushetu mpya, ya kusema na kutenda kweli. mimi sitaki maneno, nataka kusema na kutenda”,ameongeza Mayengo.
Ameeleza kuwa kama atapata ridhaa ya kuteuliwa kugombea, vipaumbele vyake ni afya, miundombinu kuunganisha kata, umeme na kilimo akisisitiza kuwa ataenda kuiunganisha Ushetu.
Mhe. Simon Makoye Mayengo akitangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Simon Makoye Mayengo akitangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Simon Makoye Mayengo akitangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Ushetu Mkoa wa Shinyanga.