Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amewakumbusha Mawakili wa Serikali juu ya wajibu wao na masuala muhimu yanayohusu majadiliano ya mikataba mbalimbali ambayo Serikali au Taasisi inakusudia kuingia au ina maslahi nayo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo tarehe 4 Juni, 2025 wakati akiwasilisha mada kuhusu mbinu za kufanya Majadiliano ya Mikataba na namna ya Kuunganisha Utaalamu wa Kisheria na Ujuzi wa Biashara kwa washiriki wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na kuendeshwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yanayofanyika Jijini Arusha.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ni muhimu kwa mawakili wa Serikali kuzingatia umakini, weledi na uzalendo wakati wanashiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali yenye maslahi Serikali na taifa kwa ujumla.
*“Kutokana na unyeti wa majukumu ya Mawakili wa Serikali katika masuala ya mikataba hivyo ni muhimu kwa Mawakili kuzingatia weledi na kutanguliza uzalendo wakati wanashiriki kwenye majadiliano ya mikataba mbalimbali.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kutoa ushauri na msaada wa kisheria kwa Mawakili wa Serikali wakati wowote ili kuwarahisishia Mawakili wa Serikali utekelezaji wa majukumu mbalimbali hususani wakati wa majadiliano ya Mikataba.
*“Sisi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu tunawaahidi ushirikiano wa kutosha mara zote mnapohitaji ushauri wa kisheria, lengo letu ni kufanya majadiliano ya mikataba mbalimbali yanakuwa na tija kwa taifa na Wananchi wake.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Bi. Asia Juma amefurahishwa na mada zilizotolewa kwenye mafunzo hayo huku akieleza kuwa mada iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewaongezea maarifa zaidi watakayowatumia katika kuboresha utendaji kazi wao.
*“Tunamshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa wasilisho lake wasilisho lililosheheni masuala muhimu kuhusiana na majadiliano ya mikataba, naamini sisi mawakili tumejifunza mengi kutoka kwenye wasilisho hilo hivyo litatusaida kuboresha utendaji kazi wetu.”* Amesema Bi. Asia
Mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali yamehudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Palamagamba J.A Kabudi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa na Mwanasheria Mkuu Mstaafu Mhe. George Masaju, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno, Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius J. Njole na viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali na Mawakili kutoka Wizara, Taasisi, Idara na Halmashauri mbalimbli nchini yalianza tarehe 2 Juni, 2025 na yanatarajia kukamilika tarehe 4 Juni, 2025.