Tanzania imetoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kuwashirikisha wanawake katika masuala ya amani na usalama ili kudhibiti migogoro ambayo vyanzo vyake vikuu ni ukabila, ubaguzi wa rangi, itikadi kali na migogoro kuhusu maliasili na mipaka.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama unaofanyika jijjini Prishtina nchini Kosovo kuanzia Juni 2 hadi 3, 2025.
Mhe. Waziri Kombo amesema kuwa, ili kuwa na Dunia yenye amani na utulivu, Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kushirikiana na nchi mbalimbali kutoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa amani duniani na kushirikisha makundi ya wanawake na vijana katika mchakato wa amani ili kuepukana na migogoro mingi ambayo husababishwa na ukabila, itikadi kali za kisisasa na kidini, kugombea rasilimali kama madini na ubaguzi wa rangi.
Mhe. Kombo ambaye alihutubia kama mzungumzaji mkuu wakati wa Jopo la majadilino kuhusu mada isemayo βUtangamano wa Amani katika Karne ya 21: Nini kinahitajika,β amesema kuwa, katika karne hii ya sayansi na teknolojia wanawake wana nafasi na umuhimu mkubwa wa kushirikishwa katika masuala ya amani na usalama tangu ngazi ya familia hadi kimataifa kwani wao ndio wahanga wakuu wa migogoro na walezi wa familia hususan pale amani inapotoweka.
Aidha, akizungumza kuhusu Tanzania, Mhe. Waziri Kombo amesema kuwa nchi hiyo chini ya Uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kulipa suala la amani na usalama kipaumbele kwa kushiriki kikamilifu katika jitihada za utatuzi wa migogoro iliyopo katika kanda na duniani kote kwa njia za amani.
Pia amefafanua kuwa, moja ya mafanikio kwa Tanzania kuwa Taifa lenye amani duniani ni jitihada zake za kuzuia migogoro kwa njia ya amani. Kuhusu vijana Mhe. Waziri Kombo ameeleza kuwa wanapaswa kujengewa uwezo na kutengenezewa ajira ili kuepuka migogoro inayotokana na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Mhe. Waziri Kombo ameongeza kusema kuwa ni vizuri Mkutano wa Tatu utoke na mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanawake na vijana wanawezeshwa na kushirikishwa kikamilifu kwenye masuala yote yanayohusu amani na usalama.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri Kombo alitumia fursa ya Jukwaa hilo kunadi vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania kwa kuwahamasisha wajumbe kutembelea vivutio hivyo ikiwemo Ngorongoro, Serengeti na Zanzibar.
Awali, akifungua mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Kosovo, Mhe. Dkt. Vjosa Osmani Sadriu ambaye ni mwanzilishi wa jukwaa hilo, amewashukuru wajumbe wa mkutano kwa kushiriki kwa wingi na kuwaeleza kuwa amefarijika kuona Dunia bado inathamini mchango wa wanawake katika masuala ya amani na usalama na kwamba nchi yake ambayo imewahi kuwa mhanga wa migogoro itaendelea kuunga mkono jitihada zozote zinazolenga kuwainua wanawake ili kuwawezesha kuchangia kikamilifu katika masuala ya amani na usalama duniani kote.
Mkutano wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ni jukwaa linalowaleta pamoja wadau wa kimataifa waliojitolea katika kuhakikisha kunakuwepo ushiriki madhubuti wa wanawake katika kuzuia migogoro, ujenzi wa amani na shughughli za urejeshaji baada ya migogoro.
Mkutano huo unaenda sambamba na Azimio Namba 1325 la Baraza la Umoja wa Mataifa la Amani na Usalama linalotimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000. Azimio hili ndilo waraka rasmi na wa kisheria unaolenga kushughulikia athari za migogoro kwa wanawake na umuhimu wa ushiriki wao katika mchakato wa amani.
βΒ