OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi nchini ni ya kuridhisha.
Prof. Nagu ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani, yenye lengo la kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za afya, lishe na ustawi wa jamii.
“Tumejionea wenyewe kuwa upatikanaji wa dawa katika kituo hiki ni wa kiwango cha juu, na hali hii siyo hapa pekee bali ni katika vituo vingi nchini. Kwa sasa tupo kwenye wastani wa asilimia 85 ya upatikanaji wa dawa katika ngazi ya afya ya msingi,” alisema Prof. Nagu.
Ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kila mwezi hutenga zaidi ya shilingi bilioni 16.6 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
Prof. Nagu amevitaka vituo vyote vya afya kuhakikisha vinatunza dawa kwa uangalifu na kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu ili kuzuia upotevu au uharibifu.
Aidha, amewahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha wanapata huduma za afya kwa urahisi mahali popote nchini pindi wanapokumbwa na changamoto za kiafya.