Balozi wa Amani Duniani na mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu kutoka mkoa wa Geita, Mess Changula, ametangaza kuwa wanatarajia kuandaa kongamano kubwa la kitaifa lenye lengo la kuhimiza na kuendeleza amani barani Afrika na nchini Tanzania kwa ujumla. Kongamano hilo, linalojulikana kwa jina la “Kongamano la Amani na Upendo kwa Taifa”, linatarajiwa kufanyika jijini Dodoma tarehe 21 mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo mkoani Geita, Changula amesema kuwa kongamano hilo linafanyika kwa ushirikiano na Jukwaa la Wazalendo Huru Tanzania pamoja na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya amani na maendeleo ya jamii.
“Amani ni msingi muhimu uliowekwa na waasisi wa taifa letu. Ni jukumu letu kama kizazi cha sasa kuhakikisha tunalinda na kuendeleza msingi huo kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema Changula.
Aidha, amefafanua kuwa kongamano hilo litaambatana na mijadala ya kina itakayowakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya amani wakiwemo viongozi wa dini, wanaharakati, vijana na wataalamu wa masuala ya kijamii. Lengo kuu ni kujadili kwa undani njia bora za kudumisha mshikamano wa kitaifa, hususan katika vipindi nyeti kama vya uchaguzi.
Changula amesisitiza kuwa kongamano hilo linatoa fursa ya kipekee kwa Watanzania kuungana na kutafakari kwa pamoja umuhimu wa kulinda amani, upendo na mshikamano miongoni mwa jamii.